Simba yaifungia kazi Power Dynamos

25Sep 2023
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yaifungia kazi Power Dynamos

KIKOSI cha Simba kimeingia kambini kujiandaa na mechi ya mkondo wa pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia utakaochezwa Jumapili (Oktoba Mosi) Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Kikosi hicho kimeingia kambini baada ya mapumziko ya siku moja tangu ilipocheza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union Alhamisi iliyopita na kushinda mabao 3-0.

Katika mazoezi ya jana kwenye Uwanja wa Mo Arena, Bunju, Dar es Salaam, wachezaji wa timu hiyo walionekana kugawanyika sehemu mbili, waliocheza dakika zote mechi ya Alhamisi waliwekwa kwenye kundi lao  na wale waliocheza kwa dakika chache na wale ambao hawakucheza kabisa waliwekwa kwenye kundi lao na kuanza mazoezi kabla ya kucheza mchezo wa wenyewe kwa wenyewe.

Makundi hayo mawili yalikuwa yakisimamiwa na kocha wa viungo, Corneille Hategikimana na Kocha Roberto Oliviera 'Robertinho'.

Akizungumza na Nipashe, Robertinho alisema wameanza rasmi kujiandaa na mchezo dhidi ya Power Dynamos na mazoezi yao yote ni kuelekea kwenye mchezo huo muhimu ambao wanahitaji ushindi tu.

"Tumeanza na programu maalum kwa wachezaji wote kwa kuvigawa katika makundi mawili, lakini kiujumla tumeanza kujiandaa na mchezo wetu wa mrudiano, tunataka kuona tunaingia hatua ya makundi," alisema Robertinho.

Aidha, alisema wapinzani wao si timu dhaifu na watakuja kwa nguvu kujaribu kulazimisha ushindi au sare yenye manufaa kwao.

"Mchezo hautakuwa mwepesi, lakini nina imani na wachezaji wangu ingawa nitamkosa Inonga (Henock), lakini waliobaki wanaweza wakanipa kile ambacho nakitaka na mashabiki wanachokisubiria," alisema Robertinho.

Inonga ataukosa mchezo huo baada ya kuumia kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Coastal union na anatarajiwa kuwa nje kwa wiki mbili.

Simba inahitaja ushindi wowote au sare isiyozidi bao 1-1 ili kusonga mbele na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi za vilabu.