Moja ya tukio ambalo haliwezi kusahaulika ni kwa wenyeji Brazil kufanikiwa kutwaa medali ya dhahabu kwa kuwafunga Ujerumanil, mechi iliyotafsiriwa kuwa ya kulipiza kisasi kutokana na taifa hilo kuwafunga mabao 7-1 kwenye hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2014.
Kumalizika kwa michezo ya Olimpiki ya mwaka huu, ndiyo kuanza kwa maandalizi ya michezo ijayo ambayo itafanyika mwaka 2020 jijini Tokyo, Japan.
Michezo hiyo ambayo hushirikisha timu kutoka mataifa mbalimbali duniani, hulenga kutoa nafasi kwa wanamichezo nyota kuonyesha vipaji vyao na hatimaye kung'arisha nchi zao.
Kwa Tanzania, imekuwa ni muda mrefu sasa kwa wanamichezo wake wanaokwenda kushiriki michezo hiyo kuonekana 'watalii' kutokana na kushindwa kunyakua medali yoyote.
Jina 'watalii' si zuri kwa sababu linatumika kuwakebehi wawakilishi hao wa nchi ambao baadhi yao wanakwenda kwenye michezo hiyo kwa kutumia tiketi za 'viti maalumu' kutoka katika Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) baada ya kushindwa kufikia viwango vilivyowekwa na kamati hiyo.
Tukumbuke kuwa ili nchi iweze kuvuna matunda 'medali' katika michezo hiyo, ni lazima tujiulize maandalizi ya wanamichezo wetu yalikuwaje?
Walipata maandalizi yanayostahili? Kuanzia kwa vyama husika vya michezo hadi serikali? Au ni kutoa lawama pale tunapoona wanamichezo hao wameshindwa kuvuna medali katika michezo hiyo yenye hadhi ya juu duniani.
Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Huu ni muda muafaka wa kujipanga kwa vitendo kwa ajili yakufanya vizuri katika michezo ijayo ambayo itafanyika kwenye taifa ambalo pia huwekeza fedha nyingi katika michezo.
Vyama vya michezo kuwa na programu na kalenda za mashindano ya kitaifa ni jambo la kawaida, tena baadhi ya vyama vimebahatika kutengeneza programu zinazofanana na nchi nyingine zilizoendelea lakini tatizo linabaki katika utekelezaji.
Viongozi wa vyama hivyo huu ndiyo muda wa kufanya mazungumzo na kampuni na taasisi mbalimbali za biashara ili kupata fedha za kusaidia gharama za kuwaandaa wanamichezo na kampuni hizo pia zikipata nafasi ya kujitangaza na si kusubiri kutoa zawadi na pongezi kwa mwanamichezo aliyefanya vizuri.
Gazeti hili linapenda kuwakumbusha wadau wa michezo kutumia muda huu wa maandalizi kusaidia wanamichezo kupata misingi sahihi na hapo ndipo watakapokwenda kwenye fainali tuhoji kwa nini wameshindwa kurejea na medali.
Pia tunapenda kuwapongeza wazazi/ walezi wa wachezaji wa kuogelea ambao mwaka huu walikwenda kushiriki michezo hiyo kwa kuchukua jukumu la kuwapeleka katika kambi za maandalizi nje ya nchi kwa gharama zao binafsi.
Hii inatia moyo na inashawishi, wazazi au walezi wengine kuiga jambo hili kwa faida ya nchi na mchezaji.
Tulishuhudia Shirikisho la Ngumi za Riadhaa (BFT) likishindwa kupeleka mabondia Cameroon kwa ajili ya kushiriki mapambano ya kusaka tiketi ya kwenda Olimipiki kutokana na kukosa nauli.
Tubadilike, ni aibu kwa taifa kama hili lenye rasilimali mbalimbali kukosa Sh. milioni 40 za kugharamia tiketi kwa mabondia, kama kweli nchi inataka kuona wanamichezo wake wanapata medali, hili lisijirudie katika kipindi cha miaka minne inayokuja.
Serikali ambao ndio mdau mkuu katika michezo, inafahamu wazi kuwa vyama vingi vya michezo havina wadhamini na maandalizi ya wachezaji wake katika kujiandaa na mashindano mbalimbali, hukumbwa na changamoto, si vibaya ikatenga fungu la kusaidia programu hiyo badala ya kusubiri kukabidhi bendera na posho, ambazo kiukweli ni ndogo na hazilingani na hadi ya michezo hiyo.
Hakuna kisichowezekana, maandalizi mazuri ndiyo njia pekee ambayo itatufanya Watanzania kutwaa medali na si jambo lingine lolote.










