Ni vita ya Mayele na Ntibazonkiza

09Jun 2023
Faustine Feliciane
MBEYA
Nipashe
Ni vita ya Mayele na Ntibazonkiza

IKIWA imebakia mechi moja ili kumaliza msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2022/2023, kiungo mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza ameamsha vita mpya ya kuwania Kiatu cha Dhahabu dhidi ya straika wa Yanga, Fiston Mayele.

 

Mkongomani Mayele ambaye amefunga  mabao 16 alikuwa hana presha yoyote ya kutwaa tuzo hiyo mpaka 'alipoamshwa' na Ntibazonkiza aliyefikisha magoli 15, baada ya juzi kupachika mabao matano Simba ikiibuka na ushinda wa 6-1 dhidi ya Polisi Tanzania.

Mabosi wa Yanga walimwacha Mayele lakini klabu hiyo imelazimika kumpandisha ndege jana mchana kuja jijini hapa ili kuuwahi mchezo wa mwisho dhidi ya Tanzania Prisons.

Mayele hakuwa sehemu ya mipango ya kikosi kilichowasili jijini hapa Jumatatu usiku kwa ajili ya kucheza dhidi ya Mbeya City, lakini kasi ya Ntibazonkiza imewafanya Yanga kumjumuisha katika mchezo wa kesho.

Awali ilisemekana Mayele alikuwa anajiandaa kwenda kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ili kujiunga na timu ya taifa.

Taarifa kutoka Yanga zinasema Mayele alitegemea kuungana na timu jana mchana na kesho atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoumana na Tanzania Prisons.

"Mayele anasafiri leo (jana) mchana, hakuwepo katika kikosi cha awali kilichokuja Mbeya lakini sasa tumeamua aje kwa ajili ya mchezo wa mwisho," alisema mmoja wa kiongozi wa Yanga.

Mayele hakuwa sehemu ya mipango ya michezo yote miwili ya kumalizia msimu inayochezwa jijini hapa.

Kuwasili kwa Mayele katika mchezo wa kesho kutakoleza vita ya kuwania tuzo ya ufungaji bora ambayo awali alionekana tayari itakwenda kwa Mkongomani huyo bila shaka lakini mabao ya Ntibazonkiza katika mchezo wa juzi yalibadilisha upepo.

Simba iliyoko katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara itamaliza msimu huu kwa kuwakaribisha Coastal Union kutoka jijini Tanga ambayo pia inahitaji ushindi ili kujiweka mahali salama zaidi.

Msimu uliopita Mayele ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kutwa tuzo hiyo, alizidiwa kwa bao moja na aliyekuwa mshambuliaji wa Geita Gold, George Mpole, aliyefikisha idadi ya mabao 17.