Simba sasa kusukwa upya michuano CAF

01May 2023
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba sasa kusukwa upya michuano CAF

WAKATI kikosi cha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa Simba kikirejea nchini jana kutoka Morocco na kupokewa kwa shangwe kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere, Afisa Mtendaji Mkuu wake, Imani Kajula,

Ameahidi kusuka timu tishio ambayo anaamini itakwenda kufuzu hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Licha ya kutolewa kwenye hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mabingwa Watetezi, Wydad Athletic Club ya Casablaca, Morocco kwa mikwaju ya penalti 4-3, wanachama na mashabiki wa timu hiyo walijitokeza kwa wingi, wakiwa na ngoma na zana zingine za muziki kwa ajili ya mapokezi yaliyowashangaza viongozi, wachezaji na makocha.

"Niseme tu, mpira wa Tanzania unapiga hatua kubwa Afrika, leo hii tumeondoka Morocco, kila mtu anaisifu Simba na kila mtu anasifu mpira wa Tanzania, lakini hili lisitufanye tukabweteka, ila tulione kama ni changamoto ya kufanya vema zaidi. Na sisi kama klabu hilo ndilo lengo letu, hii ni sehemu ya kujipimia na ninavyokwambia tunakwenda kusuka kikosi zaidi ili tuje kushindana vizuri zaidi kipindi kijacho.

"Uzuri ni kwamba michuano ya Super Cup inaanza wakati wa msimu mpya wa ligi na michuano mingine, kwa hiyo tuna ripoti ya mwalimu, wataalam wachambuzi na waangalizi wa soka kwa ajili ya kuboresho kikosi,  na tumeona kuna maeneo ya kuyafanyia kazi na tutayafanyia kazi kweli bila matatizo yoyote," aliahidi Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo mara baada ya kuwasili uwanjani hapo.

Kajula pia aliwatoa hofu wanachama na mashabiki wa Simba kuhusu taarifa za straika wao, Jean Baleke, kutakiwa na klabu kadhaa ndani na nje ya bara la Afrika, huku ikidaiwa kuwa yupo kwa mkopo kutokea TP Mazembe, akisema Baleke ana furaha ndani ya klabu hiyo, hivyo hawezi kuondoka.

"Baleke ana furaha sana Simba, anapewa nafasi, wachezaji wenzake na mashabiki wanampenda sana, unajua nao wachezaji hawa wanajua vitu vingi na wanapenda amani na faraja, niseme tu kuwa mmoja kati ya wachezaji waliolia sana tulipotolewa ni Baleke, kwa hiyo ana mapenzi makubwa na klabu, siwezi kuweka sana mambo ya mikataba, lakini yupo sana Simba," alisema.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira aliwapongeza wachezaji wake kwa kiwango kikubwa walichokionyesha kiasi kwamba mabingwa watetezi walilazimika tu kuomba Mungu ili wafuzu.

"Nawapongeza  wachezaji wangu, wamecheza kwa kiwango kikubwa, siwezi kusema kuhusu penalti, lakini kila mmoja ameshuhudia kilichotokea, kiwango cha uchezaji kwangu ndicho muhimu zaidi. Tumepambana vya kutosha, kama tungetumia nafasi mbili kubwa tulizozipata Dar es Salaam, saa hizi tungekuwa nusu fainali, lakini huu ndiyo mpira," alisema Robertinho.

Clatous Chama kwa upande wake alisema walipambana kiasi cha kutosha kwa ajili ya mashabiki, wanachama na familia zao, lakini haikuwa bahati yao.

"Hatuna cha kusema, kweli tumetoka, lakini mimi nashukuru kwa Mungu, viongozi wetu, mashabiki, familia na wote waliokuwa wanatupa sapoti, tumechoka, lakini mimi naona kama tumepambana vizuri tu, haikuwa bahati yetu ni mipango ya Mungu tu, tumshukuru Mungu. Kukosa penalti inaumiza sana, lakini ni mpira hatuwezi kusema mengi na imepita, tutaangalia yale yanayokuja mbele," alisema Chama.

Kwa upande wa Meneja Habari na Mawasiliano ya Klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema kufika hatua ya robo fainali mara tatu haina maana Simba imefeli kwa sababu Mamelodi Sundowns, timu inayosifiwa kwa ubora Afrika kwa misimu mitano imekuwa ikiishia robo fainali na sasa wamefanikiwa kutinga nusu.

“Kama Simba tumecheza robo fainali tatu tunaambiwa tumefeli vipi hao walicheza mara tano na msimu huu kufanikiwa, bado tuna sababu ya kujivunia kwa hapa tulipofikia na kusahihisha makosa yetu na kujifunza kutokana na wenzetu.

"Ili kutoka hapa lazima tufanye juhudi kila linalowezekana kufanya usajili wa wachezaji bora na wenye uwezo wa kuipeleka Simba nusu fainali,” alisema Ahmed.

Aliongeza kuwa wachezaji walipo sasa, ikija michuano hiyo mingine wanauwezo wa kuifikisha Simba robo fainali, hivyo wanalazimika kufanya usajili kwa kuongeza nyota wengine wenye uwezo mkubwa kuja kuongeza nguvu ndani ya Simba.

“Viongozi wanalijua hili na tayari mchakato umeanza mapema wa kutafuta wachezaji kulingana na mapendekezo ya awali ya benchi la ufundi kusajili wachezaji walio na uwezo bora watakaokuja kusaidiana na waliopo kikosini kuipeleka Simba nusu fainali msimu ujao,” alisema Meneja huyo wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba.

Aliwataka mashabiki kutoikatia tamaa timu yao kwa sababu Simba ni timu pekee katika Ukanda wa CECAFA inatarajia kucheza michuano ya Super League na wanaimani watafanya vizuri kwa sababu ya usajili watakaoufanya.

“Simba imekuwa timu ambayo inakatiwa tamaa tangu kuanza msimu huu maana tulivyopangwa na Nyassa Big Bullets tukaambiwa utakuwa mwisho wetu, lakini juhudi za wachezaji na kupambana tukamfunga nje ndani, hali hiyo pia kwa De Agosto, ikaja makundi hakuna aliyeipa heshima Simba na hatimaye kucheza robo.

"Licha ya kufanikiwa robo pia wakiendelea kuikatia tamaa hasa tulipocheza na Wydad Casablanca nyumbani na kushinda bao 1-0 ila hawakuishia hapo wakadai kwamba tunaondolewa kwa aibu kwa kufungwa bao nyingi, lakini kilichotokea huku Wydad Casablanca wanajua,” alisema .

Aidha, Ahmed alisema kikosi kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam leo kuelekea Ruangwa mkoani Lindi kwa ajili ya mechi ya ligi dhidi ya Namungo FC, itakayopigwa keshokutwa katika Uwanja wa Majaliwa, na nusu fainali ya Kombe la FA, Jumamosi wiki hii kwenye Dimba la Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara.