Majaliwa amewataka wakuu wa Wilaya kukaa pamoja na wafanyabiashara na kuwahimiza kushusha bidhaa zote za chakula ususani zinazozalishwa ndani kwani bei za mafuta tayari zimeshuka.
Akizungumza mara baada ya kuwasili mkoani mwanza, katika kikao cha pamoja na kamati ya Usalama Mkoa wa Mwanza, madiwani pamoja na viongozi wa chama cha mapinduzi mkoani hapa, Majaliwa amesema kuwa haiwezekani bidhaa ziendelee kupanda na kuzidi kuwaumiza wananchi.
"Nawaagiza wakuu wa Wilaya nendeni mkashughulikie hili haiwezekani hata bidhaa zinazozalishwa ndani ziendelee kupanda na mafuta yameshuka," amesema Majaliwa.
Aidha, Majaliwa amewataka viongozi mkoani hapa kuwahimiza wananchi kuongeza juhudi katika uzalishaji wa zao la chakula ili kuepusha baa la njaa kutokana na uhaba wa chakula.
Katika hatua nyingine Majaliwa amewataka viongozi wa Mkoa huo kuwa na utaratibu wa kutembelea miradi inayotekelezwa na serikali kwa kupambana na viongozi wa ngazi za vijiji ili kutangaza miradi hiyo ijulikane kwa wananchi.
"Serikali ya juu tunatekeleza miradi mingi lakini inaishia kujulikana kwa viongozi pekee tengenezeni timu ya kuzungukia miradi na kuitangaza kwa wananchi" amesema.
Pia amewataka wakuu wa Wilaya kufuatilia uongozi wa vijiji na kuhakikisha kunakuwepo na mikutano ya vijiji ambayo itaambatana na kusomwa kwa mapato na matumizi ili kuwapa nafasi wananchi kuelewa maendeleo ya vijiji vyao.
Vilevile amewataka Wakurugenzi kutoa taarifa za fedha zinazotumwa na serikali kuu kwa wakuu wa Wilaya ili kuimarisha kuaminika kwa serikali.
Majaliwa amesema kuwa Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa yenye hoja nyingi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali ambazo hazijajibiwa ukiwa na jumla ya hoja 374.
Vilevile amesema kuwa kati ya Wilaya 50 zenye hoja nyingi na hazijajibiwa, Mkoa wa Mwanza ukiwa na Wilaya tano ambazo ni kwimba hoja 70, buchosa 69, kwimba 51 ukerewe 49 na Nyamagana 45.
Amesema nje ya taarifa hizo kutokujibiwa bado mkoa pamoja na wilaya hazijachukua hatua yoyote juu ya hoja hizo huku akiwataka makatibu tawala wa mikoa pamoja na wilaya kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa majibu hayo kabla ya wakaguzi kuanza kufuatilia.
Kuhusu, utalii Majaliwa ameutaka uongozi mkoani hapa kuongeza juhudi katika kuutangaza ili kuongeza vyanzo vya mapato.
Aidha, amesema kuwa si vibaya Mkoa wa Mwanza kuzitangaza mbuga za Serengeti kwani upo uwezekano wa watalii wengi kuutumia uwanja wa ndege wa Mwanza ambapo ni karibu kuelekea mbunga hiyo maarufu.
Awali akisoma taarifa ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Kighoma Malima, ameomba serikali kutoa bajeti kwaajili ya upanuzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa mkoa hupa ambalo limesitishwa ujenzi wake kutokana na kutokutosheleza mahitaji ya mkoa.
Akiwa mkoani Mwanza Majaliwa atafanya ukaguzi maendeleo ya ujenzi wa miradi ya kimkakati kikiwemo daraja la Magufuli (Busisi-Kigongo) ujenzi wa reli ya kisasa SGR , Jengo la huduma ya macho Bugando pamoja na kushiriki ujenzi wa zahanati hatua ya msingi (kisiwani Gana) na kukagua maendeleo ya ujenzi wa meli ya Mv. Mwanza.










