Ukatili wa kijinsia tatizo kubwa

31May 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ukatili wa kijinsia tatizo kubwa

JUZI wabunge walipaza sauti kuhusu kukithiri vitendo vya ukatili nchini, vinavyogharimu maisha ya wengi huku wakiachwa na mateso kisaikolojia.

Wawakilishi wa wananchi hao walikuwa kwenye semina ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, wakitaka serikali na jamii kuja na njia za kukomesha ukatili huo kwa lengo la kuwa na kizazi chenye ustawi na kusichokuwa na maumivu kutokana na ukatili.

Katika semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, aliwaeleza wabunge walivyopokea ujumbe kutoka kwenye mkoa fulani ukieleza jinsi babu alivyokuwa akimbaka mjukuu wake kwa mwaka mmoja.

Wabunge walisema kuna ukatili mwingi unaendelea kwenye jamii na sio kila mtu anaweza kwenda kuripoti, huku wakisema idadi ya madawati yaliyoko ni ndogo ikilinganishwa na kesi.

Wapendekeza lazima kuwe na msaada wa kisaikolojia kwasababu mtoto anapofanyiwa ukatili, kuna uwezekano wa kulipiza kwa wengine baadaye.

Kila siku kuna wastani wa matukio zaidi ya mawili yakitokea mikoa tofauti, ambayo yanahusu mtoto kubakwa na mtu wa karibu au wa mbali, wakati mwingine hadi mzazi.

Tukio la juzi ni la kijana kumuua mkewe mwenye umri wa miaka 26 waliodumu kwenye ndoa kwa miezi mitano, huku Arusha kuna mtu ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa madai ya kubaka wanawake kwa muda mrefu, kisha kujipaka mafuta ili watu watakapojaribu kumkamata wasiweze kutokana na mwili kuteleza.

Zipo jitihada nyingi zimefanywa na serikali ikiwamo kuunda kamati mbalimbali, pia kuanzisha dawati la jinsia kwenye vituo vya polisi, ili iwe rahisi mtu kuripoti anapofanyiwa ukatili.

Ni lazima kufanya tathmini ya hatua zilizochukuliwa kama zimeleta matokeo sahihi au zinasaidia kwa kuwa licha ya kuwapo bado matukio yameendelea kuwapo kwa wingi na kuumiza wengi.

Kama ambavyo wabunge wameona hata watu wengine kwenye jamii wanaona na kufikiria nini kifanyike, mathalani wanasaikolojia wanaeleza sababu za watu kufikia kufanya ukatili, huku wengine wakichukua hatua ya kujiua au kuua wengine.

Watoto wanabakwa na kulawitiwa, kwenye shule za msingi na sekondari matukio hayo yanaripotiwa kwamba wanafunzi kwa wanafunzi wanafanyiana matukio hayo au kufanyiwa na walimu au wazazi wao.

Ni lazima jamii itafakari na kuchukua hatua, jambo hili sio la serikali pekee na waliotendewa ukatili huo peke yake, bali kila mwanajamii kwa kuwa kuna uwezekano wa wengi kuendelea kuumia kama hakutakuwa na hatua sahihi.

Ni muhimu vyombo vya habari vikasaidia kutoa elimu, kualika wataalamu wa saikolojia kuzungumza kwanini mtu anafikia kufanya ukatili, kuwatambua wenye matatizo ya akili na serikali kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake kwa kufungua fursa zaidi za ajira ili kupunguza makali ya maisha.