Nusu fainali ya kwanza ilipigwa Jumamosi katika Uwanja wa CCM Kirumba ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba na ya pili ikapigwa jana Jumapili kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kati ya Azam FC na Coastal Union.
Kawaida michuano hiyo huanzia ngazi ya chini kwa kuchezwa katika viwanja mbalimbali kwa kutegemeana na droo inavyochezeshwa kabla ya kutinga raundi ya 64 ambapo timu za Ligi Kuu huanza kushiriki.
Michuano hiyo huanza kuwa na msisimko mkubwa na kuvuta hisia zaidi pindi timu za Ligi Kuu zinapoingia, hiyo ikitokana na kuwa na mashabiki wengi.
Hisia, wingi na utayari wa mashabiki huongezeka zaidi inapoingia hatua ya robo fainali, nusu fainali na hatimaye fainali, ambapo bingwa huiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Inapofika hatua ya nusu fainali na fainali, TFF hupanga viwanja vya mikoani nje ya ule mkubwa nchini wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, lengo likiwa zuri tu la kutaka kupeleka soka kila kona ya nchi hususan kwa mikoa ambayo haina timu za Ligi Kuu.
Tunaelewa kabisa lengo la TFF ni zuri kwani linalenga kuchochea wadau wa mchezo huo kwenye mikoa hiyo kuona haja ya kuwa na timu za Ligi Kuu ili kupata burudani ya soka mara nyingi zaidi kwa msimu.
Lakini pamoja na lengo zuri kwa TFF, sisi tunaona ipo haja kwa sasa shirikisho hilo kubadiki utaratibu huo na kufanya kuwa kuanzia timu za Ligi Kuu zinapoingia michuano hiyo kupangwa kuchezwa viwanja vya mikoani ambazo hazina timu Ligi Kuu na inapofika hatua ya nusu fainali na fainali, kurejeshwa katika uwanja ulio bora zaidi nchini, Benjamin Mkapa.
Lakini pia kama inaona katika hatua za awali pindi zinapoingia timu za Ligi Kuu ni vigumu kufanya hivyo, basi TFF inaweza kulifanya kuanzia hatua ya robo fainali ili kufikia malengo ambayo inaona yanaweza kutimia wakifanya hivyo.
Tunaona michuano hiyo inapofika hatua ya nusu fainali, inapaswa kuchezwa katika viwanja bora viwili nchini, kwa nusu fainali moja kupigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na nyingine Benjamin Mkapa. Na hatua ya fainali ipigwe tena kwa Mkapa.
Tunasema hivyo, kwa sababu hatua hizo huvutia watu wengi zaidi kutaka kwenda uwanjani kushuhudia mubashara, lakini pia mechi kubwa kama za hatua hiyo, ndizo hutangaza soka letu pamoja na ubora wa miondombinu tuliyonayo nchini kisoka.
Tunatambua wapo watakaohoji kuwa mbona uwezo wa Uwanja wa Azam Complex nao ni mdogo, lakini hapa tumeutaja kwa kuakisi zaidi ubora wake hasa tukizingatia kuwa zipo timu kutoka nje zimekuwa zikiomba nafasi ya kuja kucheza mechi zake za kimataifa hapo na kuiingizia nchi fedha za kigeni.
Kupeleka mechi kubwa kama hizo, ambazo zinafuatiliwa na wapenda soka wengi ndani na nje ya nchi, ni kuinyima fursa Tanzania kutangaza ubora wa miondombinu ya viwanja vyetu hivyo ambavyo vinaweza kuingizia nchi mapato ya fedha za kigeni.
Lakini pia, mechi kama hiyo ambayo huvuta hisia kubwa ya mashabiki, tunaamini kwamba waliohudhuria uwanjani hata waliokuwa wakifuatikia kupitia TV hawakutendewa haki kutokana na ubovu wa uwanja, mpira kuonekana ukidundadunda jambo ambalo linapoteza raha ya mechi kubwa.
Kuiga jambo jema si dhambi, hivyo TFF haina budi kuiga ama kufuata utaratibu kama wa England ambapo michuano hiyo ya FA na ile ya Kombe la Ligi (Carabao Cup), fainali mechi hizo hupigwa Uwanja wa Wembley (Taifa).
Pamoja na England kuwa na viwanja vingi bora, hufanya hivyo, kwanza kwa sababu Wembley ni Uwanja huru (Neutral Ground), ubora na ukubwa, lakini pia hutumia fursa hiyo kuutangaza na kutangaza soka lao.
Hivyo, ni wakati sasa kwa TFF kubadili mtazamo wake huo na kutotazama faida moja tu kwenye michuano hiyo, ili kuleta ufanisi bora zaidi na mapinduzi makubwa katika soka letu.










