Mwenge wa Uhuru usivumilie miradi ya chini ya kiwango

20Apr 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mwenge wa Uhuru usivumilie miradi ya chini ya kiwango

KATIKA kuharakisha maendeleo, serikali imekuwa ikitafuta fedha hata za mikopo na nyingine za walipa kodi ili kufikia lengo hilo, kwa kujenga na kuboresha miradi mbalimbali ikiwamo midogo na mikubwa.

Pamoja na juhudi hizo za serikali, kumekuwapo hujuma zinazofanywa kwenye miradi hiyo zinazoweza kusababisha serikali isifikie kile ambacho imekusudia kukifanya kwa ajili ya maendeleo hayo.

Hiyo inajumuisha hujuma kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo chini ya kiwango, hali inayoweza kuiingiza serikali kwenye gharama zisizotarajiwa, kwa kurudia upya ujenzi wa miradi husika.

Kwa mfano, katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka jana, kiongozi huyo alikataa kuzindua miradi 52 ambayo ilitiliwa shaka kwa kuwa ilikuwa hailingani na thamani ya fedha iliyotumika kuijenga.

Ni hatua iliyoendana na agizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kufanya uchunguzi wa miradi hiyo 52 na kuwachukulia hatua mahakamani wote ambao wangebainika katika hujuma hiyo.

Wakati wa kuzinduliwa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu wa 2022 mkoani Njombe, kiongozi wa mbio hizo akakumbusha kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa ni kichocheo cha maendeleo na kudumisha umoja nchini.

Nikirejea kwenye hujuma katika miradi hiyo, ni kwamba mbio hizo zimekuwa zikiizibua kila mwaka isipokuwa mwaka 2020 ambao hazikufanyika, lakini kumekuwapo matukio ya kukataa uzinduzi wa miradi iliotiliwa shaka.

Kwa mfano mwaka 2019, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wakati huo, Mzee Mkongea Ally, akagoma kuzindua mradi wa maji uliogharimu zaidi ya Sh. Milioni 200 na wasakwe waliohusika na ubadhirifu wa fedha hizo mradi.

Nadhani kwamba kwa matukio mbalimbali ya hujuma katika miradi ya maendeleo, ingependeza kama safari hii mbio hizo zitaendelea kukwepa miradi ambayo utekelezaji wake uko chini ya kiwango.

Ninaamini kwamba, serikali inapotoa fedha kwa ajili ya maendeleo inatarajia kuona zitatumika ilivyokusudia, kwamba miradi ilingane na thamani ya fedha iliyotumika kwa usimamizi wa watendaji wa maeneo husika.

Hilo ndilo linalomfanya Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango awaagize viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru nchini, kuhakikisha hawazindui miradi watakayoibaini haiendani na thamani ya fedha iliyotumika.

Zaidi anaelekeza viongozi hao kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohusika kwa miradi mtakayoitilia shaka ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wale wote watakaobainika kuhusika na hujuma.

Pamoja na hayo, ni vyema watendaji wa serikali wasitumie vyeo vyao kwa manufaa yao, badala yake wasimamie ujezi wa miradi ya maendeleo kwa  manufaa ya maeneo wanayoongoza na taifa kwa ujumla.

Vivyo hivyo, wananchi nao kwa upande wao, wawe mstari wa mbele kufuatilia miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili waweze kubaini kama utekelezaji wake unalingana na thamani ya fedha iliyotumika.

Njia hiyo inaweza kusaidia kuziba mianya ya hujuma inayotumika kutekeleza miradi chini ya kiwango, hata kuwafanya wenye nia hiyo kuwa waoga kutumia fedha za walipa kodi kwa manufaa yao.

Wananchi wana haki ya kuhoji miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, lakini wakikaa kimya, wajanja wachache wataendelea kutumia nafasi hiyo kujinufaisha, badala ya kunufaisha taifa kwa kutekeleza miradi kikamilifu.

Iwapo watajitenga na kudhani hawahusiki kufuatilia miradi kwenye maeneo yao, ni wazi hujuma hizo zinaweza kuendelea kuwapo, hivyo ingefaa wananchi nao wafanye sehemu ya kudhibiti kila aina ya ubadhirifu.