Simba imekuwa na baadhi ya majeruhi ambao wakishaumia kupona inakuwa mtihani, wengine wakiumia mara kwa mara, kikubwa zaidi wakati mwingine wanakuwa wengi kwa wakati mmoja.
Mfano kama Chris Mugalu amekuwa ni majeruhi wa kudumu. Amekuwa kwenye chumba cha daktari zaidi badala ya uwanjani, kwani akicheza mechi mbili au tatu, basi ataumia na kurejea kwake inaweza kupita mechi sita, nane au kumi, ndipo arejee tena.
Majeruhi wengine wa mara kwa mara ni John Bocco, Thadeo Lwanga yeye aliumia na kukaa kwa muda mrefu, Mzamiru Yassin, huku mchezaji tegemeo kwa sasa Pape Sakho yeye amekuwa akiumia mara kwa mara, lakini akirejea kwa muda mfupi, tofauti na mwanzoni aliposajiliwa, na kuumia kwenye mechi za kwanza na akakaa kwa muda kidogo bila kucheza.
Kwa upande wa Yanga, kuna Kibwana Shomari, Abdallah Saibu 'Ninja', Feisal Salum 'Fei Toto', Yacouba Songne, ambaye tayari sasa ameanza mazoezi baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, Yassin Mustapha. Pia hata Djuma Shaaban. Mwingine ambaye ni majeruhi wa mara kwa mara ni Khalid Aucho.
Hivi karibuni Fei Toto aligundulika kuwa ni majeruhi kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, lakini akiwa anacheza kwenye timu yake ya Yanga.
Kama ni kweli, Fei Toto alikuwa anacheza kwenye timu yake ya Yanga akiwa ni majeruhi, basi ni jambo la hatari ambalo linaweza kumfanya awe majeruhi wa kudumu, lakini linaweza kufupisha karia yake ya soka, akiwa bado na umri unamruhusu kucheza.
Tuliona wachezaji wa zamani waliokuwa wakipigwa sindano za ganzi ili kuendelea kuzitumikia timu zao wakati wakiwa majeruhi mwisho wao wa soka haukuwa mzuri.
Na klabu zilizokuwa zikifanya hivyo, ziliwaacha na kutafuta wachezaji wengine, maisha yakaendelea.
Tukirudi kwenye mada yetu kuu, ni kwamba inawezekana kweli wachezaji wa klabu za Simba na Yanga ndiyo wanaowindwa sana na timu zingine ili kuumizwa.
Cha ajabu ni kwamba baadhi ya wachezaji wa timu hizo hizo huwa hawaumii kihivyo. Hata kama wataumizwa, basi watapata matibabu na kupona kwa muda mfupi.
Wachezaji kama Meddie Kagere, Clatous Chama, Mohamed Hussein, na wengineo hata Luis Miquissone ambaye ameondoka klabu ya Simba, ni aghalabu sana kutokea kuumizwa na kukaa nje sana, licha ya kupaniwa na wapinzani.
Fiston Mayele, Yanick Bangala, Bakari Mwamnyeto, Deus Kaseke na wengineo wa Yanga ni wachezaji sugu ambao huwezi kukuta wakiumia mara kwa mara.
Hapo ndipo tunajiuliza, tatizo ni wachezaji wenyewe wanakuja wakiwa na majeraha ya kudumu ila klabu zetu zinashindwa kuwachunguza vya kutosha, au vitengo vya tiba vya klabu za Tanzania vina matatizo?
Mimi nadhani klabu hizi zianze kuwafanyia uchunguzi wa kina wachezaji wa nje na wa ndani ambao inataka kuwasajili, badala ya kuwa na mihemko tu ya kumhitaji mchezaji fulani kuogopa atachukuliwa na timu nyingine, hivyo kuwahi kumsajili.
Wengine wanakuwa na majeraha ya kudumu, hivyo baadaye kuzigharimu timu, kwa kupata mishahara ya bure huku wakikaa muda mrefu bila kucheza.
Huwezi kukuta kitu kama hicho Azam FC, pamoja na matatizo waliyonayo, lakini kwenye suala la kuchunguza afya za wachezaji wapo vizuri. Hawachunguzi kwa fasheni. Ndiyo maana imekuwa ni timu iliyowapeleka wachezaji wengi nje ya nchi kuwatibia.
Wachezaji nao wana tabia ya kudanganya umri, hivyo vitengo vya tiba huwapatia dawa kulingana na umri walioutaja, hivyo kusababisha wasipone upesi wanapokuwa na majeraha.
Ni wakati sasa wa klabu kuimarisha vitengo vyao vya tiba ili kutoingizwa mkenge na baadhi ya wachezaji wenye majeraha ya kudumu ambao wanaonekana kama wanakuja kujiunga na timu za Tanzania kama sehemu ya kupumzika tu na kupiga hela si kucheza soka.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








