Nikatoa mifano kadhaa ya watu waliofanikiwa katika maisha kwa kushirikisha watu wengine. Nikamtaja mmojawapo kuwa ni Bill Gates, tajiri mkubwa toka Marekani, mwanzilishi wa kampuni kubwa ya Microsoft.
Vilevile, nikaanza kutaja mambo kadhaa ya kuzingatia endapo unataka kufanikisha malengo yako. Nikasema tafuta washirika waaminifu na watii. Pia tengeneza mfumo madhubuti wa utendaji ambao ukizingatiwa utaleta mafanikio.
Kingine cha kuzingatia ni kwamba, tafuta washirika au marafiki wenye ujuzi na uzoefu. Ili upate mafanikio ni vema kuanza vema, ukikosea mwanzoni itakuwa vigumu sana kujisahihisha baadaye.
Hii itakuepushia makosa mengi hapo mwanzoni na kukupa wepesi wa kuendelea mbele kwa uhakika. Unapokuwa na marafiki na washirika wenye ujuzi na uzoefu itakuwezesha kufahamu mambo mengi kabla hata haujaanza shughuli yenyewe. Hii ni sawa na kufaulu kwa asilimia hamisi tayari.
Inawezekana shughuli unayotaka kuifanya huna ujuzi wala uelewa wa kutosha, hivyo ni muhimu kuwapata wenye sifa kwani hao watakusaidia hata wewe kukupa uzoefu.
Wapo watu wana mtizamo kwamba siyo sahihi kuanzisha shughuli ambayo huna ujuzi au uzoefu nayo. Msimamo huu siyo sahihi kwani lengo siyo wewe kufanya kila kitu mwenyewe. Kumbuka kwamba unalolifanya ni matokeo ya maono Mungu aliyokupa.
Kuna watu walioanzisha biashara ambazo hawakuwa na ujuzi nazo kabisa, lakini walifanikiwa kupata wenye ujuzi wachache wakashirikiana na baadaye kufanikiwa sana.
Jack Ma, aliyeanzisha mtandao wa masoko uitwao Ali Baba, hakuwa na ujuzi wala uzoefu. Alipata washirika wachache wenye ujuzi wa programu za kompyuta na leo amekuwa tajiri mkubwa kuliko wote nchini China.
Huwezi kuwa na ujuzi wa kila fani. Tafuta washirika wenye ujuzi na uzoefu ambao wewe huna na maono yako yatafanikiwa.
Lingine la kuzingatia ili kufanikisha malengo yako ni kutafuta marafiki wenye moyo wa kujitolea. Upo msemo kwamba ‘mwanzo ni mgumu’ na kwamba bila moyo wa kujitolea utashindwa mapema sana.
Kupata watu walio tayari kujitolea ni changamoto katika ulimwengu ulioweka pesa mbele. Washirika au marafiki wanaoweka pesa mbele hawafai kushirikiana nawe katika maono yako kwani hawa ni mamluki !
Marafiki wa aina hii ni wepesi kuiba na hata kuuza siri za shughuli zako. Watu walioweka fedha mbele hawajali kama shughuli yenu inafanikiwa au la. Tena ni wavivu na wazembe.
Ni kheri kuanza na watu wachache wanaoelewa umuhimu wa kujitolea kuliko kundi kubwa la watu walioweka maslahi yao binafsi mbele.
Wenye moyo wa kujitolea ni wavumilivu huku wakijua kwamba upo wakati wa kupanda, kupalilia, kuweka mbolea na kusubiri mavuno.
Eneo lingine la kuzingatia kufanikisha malengo yako ni kushirikiana na rafiki mwenye ujasiri wa kukwambia ukweli. Ukweli unauma lakini huponya pia. Anayekupenda kweli na kukutakia mafanikio atakwambia ukweli kwa upole na bila kumung’unya. Wengi wetu hatupendi kuambiwa ukweli hasa tunapokosea kwani tunamuona aliyetuambia ukweli kama adui.
Wale unaoshirikiana nao wakiwa na ujasiri wa kusema ukweli na wewe kuwa tayari kusikiliza, utafanikiwa katika maono yako. Usishirikiane na kundi la wanafiki, watu ambao wanalolisema siyo lile wanalolikiri mioyoni mwao.
Jiulize sana aina ya rafiki ambaye kila wakati hukubaliana nawe na kukusifia tu na hata siku moja hakukosoi wala kukusahihisha. Pia tafuta washirika wenye ubunifu. Wapo watu ambao Mungu amewapa vipawa vya ubunifu. Shirikiana na watu kama hao na siyo kuwaonea wivu na kuwakatisha tamaa. Wapo watu waliobuni vitu mbalimbali kwa faida ya nchi yetu lakini hawakusaidiwa kujiendeleza.
Ili maono ya Mungu aliyokupa yafanikiwe, atainua watu wenye vipawa mbalimbali ili ufanye nao kazi. Ingawa maono umepewa wewe haimaanishi una uwezo wa kufanya kila kitu.
Mpenzi msomaji, Waingereza wanao msemo kwamba ‘ukitaka kupata rafiki, kuwa rafiki’. Ili kupata rafiki ni muhimu wewe mwenyewe kuwa rafiki. Hali hiyo itawavuta watu wengine kushirikiana nawe.
Mpenzi msomaji, bila shaka umejifunza jambo hapo. Niishie hapa tukutane tena wiki ijayo panapo majaliwa. Ukiwa na maoni, kisa, tuma ujumbe mfupi kupitia 0715268581.

.jpg?itok=nfwjwDzv)









