TPLB msiogope lawama kufungia viwanja vibovu

17Jan 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
TPLB msiogope lawama kufungia viwanja vibovu

UWANJA wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani umefungiwa na Bodi ya Ligi nchini (TPLB), kutumika kwenye mechi za Ligi Kuu hadi hapo utakapofanyiwa marekebisho kwenye sehemu ya kuchezea 'pitch'.

Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi, ikisema tatizo kubwa linalotakiwa lifanyiwe kazi ni uwanja huo kusawazishwa vizuri na majani yake kustawishwa vema ili kuendana na matakwa ya kanuni na sheria namba moja ya soka inayozungumzia uwanja hususan eneo la kuchezea.

Ikumbukwe kuwa uwanja huo hutumiwa na timu ya Ruvu Shooting kama dimba lake la nyumbani.

Kwa maana hiyo, Bodi ya Ligi imesema kuwa timu hiyo sasa italazimika kuutumia Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kama wa nyumbani hadi hapo ule wa Mabatini utakaporekebishwa.

Hivi karibuni TPLB iliufungia Uwanja wa Manungu Complex, uliopo Turiani mkoani Morogoro kutokana na kutokidhi matakwa kama hayo.

Na hii ilikuwa ni wiki chache tu baada ya kuufungulia. Kabla ya hapo uwanja huo ulikuwa umefungiwa na kutotumika kwa kiasi cha misimu miwili kutokana na kutokidhi matakwa ya kuuzungushia ukuta.

Pamoja na kwamba tayari umeshazungushiwa ukuta, bado haujamalizika vizuri, lakini kuna matatizo kwenye sehemu ya kuchezea, picha za televisheni wakati timu inayotumia uwanja huo Mtibwa Sugar ilipokuwa inacheza mechi yake ya Ligi Kuu, ilionekana kuna sehemu hakuna nyasi, zingine zipo, kiasi cha kuchekesha hata watu waliokuwa wakitazama mechi hiyo, kwani ilionekana ni kama shamba lenye vitalu.

Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiilaumu Bodi ya Ligi kwa kudai ni kwa nini wanavifungia viwanja hivyo baada ya kuona ubovu kwenye televisheni? Wengine wanadai kwani huwa havikaguliwi mwanzo? Nani alivikagua? Na kwa nini kuna wakati vinaruhusiwa na baadaye TPLB hiyo hiyo inayoviruhusu inakuja kuvifungia?

Haya ndiyo maswali na malalamiko ya wadau wa soka kwenye mitandao ya kijamii na katika mijadala mbalimbali ya michezo mitaani, redioni na kwenye televisheni.

Ukweli hapa ni kuwa, uwanja wa soka ni kama shamba, nyumba au binadamu. Ni leo inaweza kuwa hivi, lakini kesho ikawa vile. Binadamu anaweza kuamka leo mzima, kesho akawa mgonjwa.

Viwanja hivi awali huwa vinakaguliwa kabla ya kuanza ligi, na haiwezekani wakaguzi wakavikagua Agosti, basi vikabaki na ubora huo huo hadi Desemba au Januari. Hapa katikati vinatakiwa viendelee kutunzwa na wasimamizi wa viwanja.

Kuna ukame, matunzo mabovu na mvua kupita kiasi pia, vyote hivi vinasababisha ubovu wa uwanja. Na kama hatutokuwa na usimamizi mzuri uwanja hauwezi kuwa vile vile kama ulivyokaguliwa mwanzo. Na haiwezekani bodi iwe inasafirisha watu wake kukagua viwanja kila kabla ya mechi za Ligi Kuu kuchezwa.

Ndiyo maana unaona Bodi ya Ligi nayo wakati mwingine inatumia televisheni kuangalia uwanja uko kwenye hali ile ile kama ulivyokaguliwa na kama wakiona kuna tatizo wanaufungia.

Binafsi naipongeza Bodi ya Ligi kwa hatua inazochukua mara kwa mara kuvifungia kwa sababu lengo si kukomoana, ila ni kuviboresha kwa sababu vikiboreshwa havitakuwa vya TPLB bali vya wamiliki wenyewe.

Ndiyo maana tumeona kwa mara ya kwanza Uwanja wa Manungu Complex umezungushiwa ukuta na utabaki kuwa ni mali yao, lakini jitihada zimefanywa na Bodi ya Ligi ili uwe hivyo. Na kwa bahati nzuri ni wepesi wa kufungulia viwanja mara vinapoonekana kukidhi vigezo wanavyovitaka.

Kwa hali yoyote hapa wa kulaumiwa kuhusu ubovu wa viwanja na kusababisha vifungiwe ni wamiliki wenyewe wa viwanja na si TPLB inayovikagua, kuvifungia na kuvifungulia.

Wenyewe huwa wanavikagua, lakini baadaye vinaharibika kwa sababu mbalimbali, hilo sasa linakuwa si jukumu lao tena. Na ni upotevu wa raslimali fedha kuanza kuvifuatilia kila uchao, wakati wamiliki wamekaa tu hawajali hadi wafungiwe.