Mkapa amhakikishia Rais Magufuli ushirikiano

08Jan 2016
Nipashe
Mkapa amhakikishia Rais Magufuli ushirikiano

Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, amemhakikishia Rais Dk. John Magufuli, kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wakati wote ama kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo.

Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa

Mkapa alitoa kauli hiyo jana baada ya kukutana na Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumtakia heri ya Mwaka Mpya.

Akizungumza baada ya mazungumzo na Rais Magufuli, Mkapa alisema pamoja na kumtakia heri ya Mwaka Mpya, lakini ni kumpongeza kwa dhamana aliyopewa na Watanzania kuiongoza nchi na kuunda serikali.

Alisema amemhakikishia Rais Magufuli kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wakati wote ama kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo.
Kadhalika, Rais alikutana na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, Ikulu jijini Dar es Salaam. Kwa upande wake, Jaji Warioba pamoja na kumtakia heri ya Mwaka Mpya, amempongeza Rais Magufuli kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri hususan katika kusimamia ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo muhimu ambayo yanawahusu wananchi yakiwamo ya afya na maji.

Jaji Warioba aliongeza kuwa Watanzania wote wanapaswa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi kubwa anazofanya, ambazo ni kukomesha rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na wizi wa mali ya umma.