Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison amesema kwa sasa wamesahau kila kitu, akili yao ipo katika mechi nne mfululizo ambazo watacheza kuanzia Ijumaa ijayo dhidi ya Namungo FC, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi, lakini pia wana mechi ngumu dhidi ya Ihefu FC na Azam FC.
“Kwa sasa Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, akili yake ni kuwaandaa vijana kwa ajili ya mchezo wa Ijumaa dhidi ya Namungo, na tunakuwa na mechi nne mfululizo, kwani Machi 11 tutakuwa nyumbani kuikaribisha Ihefu, Machi 14 tutacheza dhidi ya Geita Gold hapa hapa nyumbani, tarehe 17 Machi tutakuwa Azam Complex kucheza dhidi ya Azam FC, ni mechi ngumu na zipo karibu karibu, hivyo inahitaji umakini na maandalizi mazuri,” amesema Harrison.
Yanga imekuwa ikipata upinzani mkali inapocheza dhidi ya Ihefu FC hasa inapocheza ugenini kwani katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliangukia pua kwa kichapo cha mabao 2-1, mechi iliyochezwa, Oktoba 4, mwaka jana katika Uwanja wa Highland Estates, Mbarali, Mbeya, lakini kwa sasa imehamia Singida.
Hata hivyo, mechi hiyo itachezwa jijini Dar es Salaam, ambapo angalau hupata unafuu. Pamoja na kupata matokeo mazuri mara kwa mara dhidi ya Azam, lakini pia hupata upinzani mkali, huku mechi baina yao ikizalisha mabao mengi kwa kila timu.
Mara ya mwisho zilipokutana katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Oktoba 23, mwaka jana, Yanga ilipata ushindi wa mabao 3-2. Wakati meneja huyo akisema hayo, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema licha ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, hawatoidharau timu yoyote ile watakayokwenda kucheza nayo, wala Ligi Kuu yenyewe.
“Nawaambia mashabiki na wanachama wetu, pamoja na kwamba tumetinga hatua ya robo fainali na sasa bado tupo kwenye furaha, lakini sasa akili yetu tuipeleke kwenye mechi za Ligi Kuu. Kuanzia wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na mashabiki, akili na nguvu zetu tuzielekeze huku kwa sababu ni muhimu sana.
Ni muhimu sana, tunaanza na Namungo Ijumaa, kwa hiyo ni lazima tuwekeze nguvu zetu hapo tuweze kufanya vizuri, kwa sababu huku ndiko kunatupa nafasi na tiketi ya kucheza mechi za kimataifa, bila ya kupata nafasi za juu huku kwenye ligi huwezi kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, hatuidharau timu wala ligi yenyewe,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa hata kama timu ikitwaa ubingwa wa Afrika, lakini kama haikupata nafasi kwenye ligi yake ya nyumbani msimu ujao haiwezi kushiriki na hilo linawafanya wawe makini zaidi kwa sasa katika mechi hizo.
Yanga ambayo ndiyo bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, pia ni vinara wakiongoza wakiwa na pointi 43 sawa na Azam FC kwa sasa, lakini wako pungufu kwa michezo mitatu.
Inaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, ikiwa imecheza mechi 16, Azam ikifikisha michezo 19 mpaka sasa.