Ushindi huo wa Yanga umeifanya kufikisha pointi 71 na hivyo inahitaji pointi tatu ili ifikishe pointi 74 tu kujihakikishia taji hilo kwa sababu hakuna timu yoyote inayoweza kufikia idadi hiyo.
Simba iliyoko katika nafasi ya pili na pointi 64 mkononi, endapo itashinda mechi zake tatu zilizobakia itafikisha pointi 73.
Stephano Aziz Ki aliendelea kuwa mwiba kwa magolikipa kutokana na mashuti yake baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya 15 kufuatia shuti kali lililomshinda golikipa wa Singida BS, Benedicto Haule kulidaka.
Baada ya kuingia bao hilo, Yanga waliendelea kulisakama lango la wapinzani wao na dakika tano baadaye, Clement Mzize, alitumia vyema krosi ya Jesus Moloko kuandika goli la pili katika mchezo huo.
Mabao hayo yalidumu kipindi chote cha kwanza, kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikifanya mabadiliko, Singida BS wakimtoa, Meddie Kagere na kuingia Enock Agyei huku Yanga wakiwatoa kwa nyakati tofauti MoLoko, Mzize na Aziz Ki na nafasi zao kuchukuliwa na Bernard Morison, Salum Abubakary 'Sure Boy' na Fiston Mayele.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadili matokeo ya mchezo, zaidi ya wenyeji kujipanga kuzuia mashambulizi yaliyokuwa yakitengenezwa na Yanga.
Pamoja na juhudi za safu ya ushambuliaji ya Singida Big Stars kuweza kupata goli, juhudi hizo zilikuwa zikiishia kwenye safu ya mabeki wa Yanga iliyokuwa chini ya Bakari Mwamnyeto na kipa, Djigui Diarra.
Baada ya mechi hiyo, Yanga ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa wataanza kujiandaa na mchezo wake wa kwanza wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mallumo Gallants ya Afrika Kusini utakaochezwa Mei 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Wakati huo huo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyokutana jana ilitumia dakika 27 kusikiliza shauri la Fei Toto na Yanga ambao walipeleka pingamizi la kutaka mchezaji huyo kuvunja mkataba kupitia klabu yao na sio shirikisho.
Fei Toto alifika TFF saa 9: 50 Alasiri na gari aina ya Toyota Alphard namba T564 ECM akiambatana na Wakili, Fatuma Karume 'Shangazi', Jasmin Razack, wakiambatana na mama yake mzazi wa mchezaji huyo.
Yanga ndio walikuwa wa kwanza kufika katika ofisi hizo wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine, Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga, Patrick Simon na wanasheria wengine.
Mwanasheria wa Yanga, Simon alisema baada ya kamati kusikiliza hoja zao na kusubiri uamuzi na anaimani suala hili kwa Tanzania limekwisha baada ya kusikilizwa zaidi ya mara tatu.
“Jambo hili limekwisha kwa hapa Tanzania, kama wanahitaji basi linaweza kuamuliwa CAS, kwa hatua hii hamashauri arudi tu kambini na aje tukae mezani ili kuboresha kile ambacho anakihitaji,” alisema Simon.
Naye Fatma Karume alisema waliambiwa walete utetezi kwa maandishi na walifanya hivyo.
“Ninaimani hoja hizo zitafanyiwa kazi, lakini dakika 10 ambazo tumepewa huwezi kuongea hoja ya msingi, huwezi kufafanua hoja hizo, wanasema watatoa uamuzi wao, hivyo tunasubiri, lakini kwa kauli ya kwenda CAS, kwa sababu akishindwa ndio anatakiwa kwenda huko, je, kwa kauli hiyo inamaana wao ndio wameshinda,” alihoji Fatma Karume.










