Yanga waitikisa TP Mazembe

25May 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Lete Raha
Yanga waitikisa TP Mazembe

YANGA imepangwa kundi la A katika Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na mabingwa wa zamani barani, TP Mazembe ya DRC, MO Bejaia ya Algeria na Medeama ya Ghana.

kikosi cha yanga kikifanya mazoezi

Kundi B linaundwa na timu za Kaskazini mwa Afrika tupu ambazo ni Etoile du Sahel ya Tunisia ambao ni mabingwa watetezi, Ahly Tripoli ya Libya, FUS Rabat na Kawkab zote za Morocco.

Mechi za mzunguko wa kwanza zitachezwa Juni 17, mwaka huu na ratiba hiyo inamaanisha Yanga itakutana na timu ya mshambuliaji wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu wa TP Mazembe ya DRC.

Na mkutano huo umemshitua Ulimwengu, ambaye ameiambia Lete Raha kwamba Mazembe wana kibarua kizito mbele ya Yanga.

“Mimi nafurahi kuja kucheza nyumbani na pia ninawapa hongera Yanga kwa kufika hatua ambayo timu nyingi zinapenda kufika. Na nina imani mchezo utakua mzuri,” alisema Uli maarufu kwa jina la Rambo mjini Lubumbashi.

Kwa upande wake, kocha Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm, alisema wamepangwa kwenye kundi gumu dhidi ya mabingwa mara tano wa Afrika, Mazembe na timu nyingine machachari MO Bejaia na Medeama ya Ghana, lakini watapambana kupata matokeo mazuri.

“NInaifahamu Mazembe, na kabla ya kuja hapa nilikuwa ninafanya kazi Ghana, Medeama ninaijua vizuri, hii MO Bejaia ni timu inayoibuka vizuri kwenye michuano ya Afrika sasa. Hakuna timu ya kubeza hapa,” alisema.

Kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima, anayechezea Yanga alisema kwamba sasa wana uzoefu wa kutosha wa mashindano makubwa baada ya kucheza mfululizo, hivyo hawaihofii timu yoyote waliyopangwa nayo.

“Katika kipindi cha miaka hii mitatu tumecheza na timu za kaskazini mwa Afrika, kusini na huku kwetu mashariki, bahati mbaya hatujakutana na timu za magharibi ambazo kwa sasa si tishio,”alisema Niyonzima.

Yanga itafungua dimba dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia nchini Algeria Juni 17, mwaka huu siku ambayo, mabingwa wa zamani wa Afrika, TP Mazembe ya DRC watakuwa wenyeji wa Medeama ya Ghana katika mchezo mwingine wa kundi hilo.

Mechi za Kundi B siku hiyo; Kawkab Marakech watakuwa wenyeji wa mabingwa watetezi Etoile du Sahel katika mchezo wa Kundi B nchini Morocco, wakati F.U.S Rabat watakuwa wenyeji wa Ahly Tripoli nchini Morocco pia.

Ikitoka Algeria, Yanga itarejea nyumbani kuikaribisha TP Mazembe Juni 28, kabla ya kumaliza na Medeama ya Ghana Julai 15, Dar es Salaam pia katika mechi za mzunguko wa kwanza.

Mzunguko wa pili, Yanga itaanzia Ghana dhidi ya Medeama Julai 26, kabla ya kurudi nyumbani nyumbani tena na MO Bejaia Agosti 12 na kasha kwenda kumalizia Lubumbashi dhidi ya TP Mazembe Agosti 23.
Timu mbili za juu katika kila kundi zitaingia nusu-fainali.

Katika habari nyingine, timu ya Mamelodi Sundowns imerejeshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kuenguliwa kwenye mashindano hayo kwa klabu ya AS Vita ya Congo kwa kumchezesha mchezaji asiyestahili.

Miamba hao wa Afrika Kusini walianza kampeni za mwaka huu kwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini wakaangukia kwenye Kombe la Shirikisho (kama Yanga) baada ya kutolewa dhidi ya Vita katika hatua iliyopita ya mtoano.

MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO
Kundi A: Yanga, TP Mazembe (DRC), MO Bejaia (Algeria), Medeama (Ghana)
Kundi B: Etoile du Sahel (Tunisia), FUS Rabat (Morocco), Kawkab Marrakech (Morocco), Ahly Tripoli (Libya)

MAKUNDI LIGI YA MABINGWA AFRIKA
Kundi A: Zesco (Zambia), Ahly (Misri), ASEC Mimosas (Ivory Coast), Wydad Athletic (Morocco)
Kundi B: Enyimba (Nigeria), Zamalek (Misri), ES Setif (Algeria), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)

RATIBA YA MECHI ZA YANGA
KUNDI A:
Juni 17, 2016
MO Bejaia Vs Yanga SC
Juni 28, 2016
Yanga SC vs TP Mazembe
Julai 15, 2016
Yanga SC Vs Medeama
Julai 26, 2016
Medeama Vs Yanga SC
Agosti 12, 2016
Yanga SC Vs MO Bejaia
Agosti 23, 2016
TP Mazembe Vs Yanga SC