Akizungumza jana, Katibu wa Baraza hilo, Ibrahim Akilimali, alisema hadi sasa wanachama wa klabu hiyo hawajui hatma yao katika kuelekea uchaguzi huo kutokana na kundi kubwa kuwa na kadi za Benki ya Posta huku TFF ikitangaza katika uchaguzi huo zitumike kadi zenye sahini za viongozi.
Alisema kutokana na utata huo, wamepeleka maombi yao kwa Serikali kupitia kwa Baraza la Michezo (BMT) kuurudisha uchaguzi huo kwa Sekretarieti ya klabu hiyo.
"Hatupingani na Serikali au TFF, lakini ukweli ni kwamba kuna utata mkubwa kuelekea kwenye uchaguzi wetu, kama tutatumia kadi za zamani, sasa hawa wanachama wenye kadi za benki ya Posta watafanyaje," alisema Akilimali.
Aidha alisema kuwa wameomba kufanyika kwa mkutano mkuu wa wanchama haraka ili kujadiliana suala hilo.
"Hatuna lengo la kuona amani ndani ya klabu yetu inaondoka, tunaomba katika mkutano huo pia wawakilishi wa BMT,TFF na DRFA (Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam) mwahudhurie," aliongeza kusema Akilimali.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, aliiambia Nipashe kuwa uchaguzi huo wa Yanga utafanyika kwa kufuata maelekezo waliyoyatoa wali.
"Timeshatoa maelekezo ambayo ndio agizo la Serikali, kwa hiyo hakuna mabadiliko na kama mnavyojua mchakato umeshaanza," alisema Mweisgwa.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF wanaosimamia uchaguzi huo, Aloyce Komba, alisema kuwa kamati yake inaendelea na mchakato wa uchaguzi huo na kusisitiza kutumia kadi za zamani pamoja na katiba ya mwaka 2010.
Nafasi zinazowaniwa katika uchaguzi huo ambao ni pamoja na Mwenyekiti,Makamu Mwenyekiti na nafasi nane za wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo.










