Al Merrikh ya Sudan itawakaribisha Yanga katika mechi ya kwanza ya hatua ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Septemba 16, mwaka huu kwenye uwanja wa Pele Nyamirambo ulioko nje kidogo ya Kigali.
Waarabu hao wamechagua kutumia uwanja huo ili kujiepusha na hali ya machafuko yaliyoko Sudan kwa sasa.
Gamondi alisema ubora wa wachezaji wake umeongezeka na kalenda ya mapumziko ya kimataifa kwake ilikuwa na faida.
Kocha huyo alisema kwa sasa kila mchezaji anafahamu majukumu yake na wanaonyesha wanakiu ya kusaka matokeo chanya katika mechi hiyo ya kwanza ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.
"Tuko tayari, tumefanya mazoezi yote muhimu kwa kuangalia mapungufu yaliyojitokeza katika mechi zilizotangulia, nimeona mabadiliko makubwa kwa kila mchezaji," alisema Gamondi.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, alisema zaidi ya mabasi 26 yatakayobeba mashabiki yataondoka nchini na kuelekea Rwanda kwa lengo la kwenda kushuhudia mchezo huo.
Kamwe alisema bado mashabiki wanaendelea kukata tiketi na kitendo hicho anaamini kitawashangaza wapinzani wao.
"Kuna mwitikio mkubwa wa mashabiki, wapinzani wetu Al Merrikh hawataamini watakachokishuhudia ndani na nje ya Uwanja wa Pele, Yanga inakwenda kuujaza uwanja huo na tumejipanga kucheza mpira mkubwa," alisema Kamwe.
Alisema mashabiki watakaokwenda Rwanda wanatoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga, Kigoma na Mwanza na kuongeza hali hiyo itawathibitishia wapinzani wao na Wanyarwanda namna Watanzania ni watu wanaopenda soka.
"Nakwambia mashabiki wa soka Rwanda, wapinzani wetu Al Merrikh nao hawataamini pale watakapoona msafara wa mabasi utakaoingia huko pamoja na kwenda kuujaza uwanja na hilo ndilo lengo letu kubwa, tutaujaza uwanja na kushangilia kama tupo nyumbani, na soka kubwa tutalionyesha," Kamwe alitamba.
Aliongeza baadhi ya wachezaji wa Yanga pia walitaka wasafiri kwa njia ya barabara na mashabiki wao lakini hilo halitawezekana kwa sababu za kiitifaki.
"Nimezungumza na wachezaji wetu (Dickson Job, Aboutwalib Mshery, Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua, wao walitaka kusafiri na mabasi ya mashabiki wetu lakini haiwezekani kiprotokali, hivyo wamewaomba mashabiki wawashangilie kwa nguvu na wao watawalipa kwa kucheza soka safi na kupata ushindi ugenini kwa ajili ya kurahisisha kazi nyumbani," alisema ofisa huyo.
Baada ya mechi hiyo ya Jumamosi, Yanga itarejea nyumbani na kuwasubiri Wasudan hao kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaochezwa Septemba 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Yanga imeendelea kutoa dozi baada ya kupata ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Kiluvya FC katika mechi ya kirafiki iliyofanyika kwenye Uwanja wa Avic Town ulioko Kigamboni jana.
Hafiz Konkoni na Kennedy Musonda kila mmoja amefunga mabao mawili katika mchezo huo wakati mengine yalipachikwa na Farid Mussa na Crispin Ngushi huku Maxi Nzengeli akitoa 'assist' ya tatu.









