NI rasmi sasa Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, watacheza mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merreikh ya Sudan.
Hatua hiyo ni baada ya kuinyoa Asas FC ya Djibouti kwa mabao 5-1 katika mchezo wa marudiano hatua ya awali ya michuano hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo ya hatua ya awali, Yanga imesonga mbele kwa jumla la mabao 7-1 kutokana na Jumapili iliyopita kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa pia kwenye uwanja huo kufuatia Asas FC kuomba kuutumia kama uwanja wake wa nyumbani.
Yanga itacheza na El Merreikh kutafuta tiketi ya kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo na mchezo wa kwanza utachezwa Septemba 15 Yanga ikianzia ugenini na kurudiana Dar es Salaam Septemba 29.
El Merreikh imeingia hatua hiyo baada kuitoa Otoho d'Oyo ya Congo Brazaville ikilazimisha sare ya bao 1-1 ugenini na kusuluhu juzi kwenye Uwanja wa Huye, Butare nchini Rwanda ambako inatumia kama uwanja wa nyumbani kutokana na machafuko nchini Sudan, hivyo imefuzu kwa bao la ugenini.
Yanga imepata ushindi mwingine wa mabao matano siku chache tu baada ya Jumatano iliyopita kuisulubu KMC mabao 5-0, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa katika uwanja huo huo.
Walikuwa wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu, Maxi Nzengeli aliyefunga mabao mawili, Hafiz Konkoni, Pacome Zouzoua, na moja la mchezaji mzawa aliyetokea benchi kwenye mchezo wa jana Clement Mzize waliopeleka kilio cha mabao hayo.
Yanga ilianza mechi kwa kasi na iliwachukua dakika moja kufanya shambulizi la nguvu kwenye lango la wapinzani wao, pale Jesus Moloko alipoondoka na mpira kwenye wingi la kulia na kupiga krosi iliyounganishwa kwa mguu wa kushoto na Stephane Aziz Ki lakini ukatoka pembeni kidogo ya lango.
Asas ilijibu shambulio hilo dakika ya tano baadae pale krosi ya Youssouf Abdi Ahmed wingi ya kulia ilipounganishwa kwa kichwa na Abbas Abdourahman, lakini mpira ukapaa juu ya lango la Yanga.
Yanga ilipata bao la kwanza dakika ya saba likifungwa na Maxi Zengeli , akiunganisha kwa kichwa krosi kutoka kwa Moloko.
Bao hilo lilitokana na wachezaji wa ASAS kujichanganya wenyewe kuokoa mpira ambao uliwakuta wachezaji wa Yanga walioupora na kutengeneza shambulizi hilo.
Dakika tatu baadae Aziz Ki alikaribia kuipa Yanga bao la pili lakini shuti lake la kushtukiza lilipaa juu kidogo ya lango la Asas FC.
Baada ya hapo ni kama Yanga iliridhika na kupunguza kidogo mashambulizi, huku wageni wao wakionekana kutulia na kucheza pasi fupi fupi ambazo hata hivyo hazikuwa na msaada mkubwa kwao wala madhara kwa wenyeji wao.
Mshambuliaji mpya wa Yanga, Konkoni alikosa bao la wazi dakika ya 21 alipobaki yeye na kipa Innocent Mbonihankuye, lakini shuti lake lilitoka sentimeta chache nje ya lango.
Wadjibouti walikosa bao dakika ya 40 kupitia kwa beki wa zamani wa Simba Gilbert Kaze ambaye alikuwa nahodha katika mchezo huo.
Kaze anakumbukwa na mashabiki wa Simba aliposawazisha kwa kichwa bao la tatu dakika ya 84 katika mechi ya watani wa jadi ya Ligi Kuu iliyochezwa Oktoba 20, 2013 Uwanja wa Benjamin Mkapa, timu hizo zikitoka sare ya mabao 3-3, Yanga ikitangulia kufunga mabao matatu kipindi cha kwanza na Simba kusawazisha yote kipindi cha pili.
Zouzoua aliyeingia kipindi cha pili alipachika bao la tatu dakika ya 54, alipowalamba chenga mabeki wa ASAS na kipa wao kabla ya kuujaza mpira wavuni.
Kipa Mbonihankuye aliumia katika purukushani hiyo, na akaingia Liban Said ambaye aliruhusu mabao mawili ya Mzize dakika ya 68 aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Nickson Kibabage, kabla ya Nzengeli kufunga bao la tano na la pili kwake katika dakika za nyongeza.
ASAS ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 83 lililofungwa na Tito Mayor kwa mkwaju wa penalti baada ya yeye mwenyewe kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mtokea benchi Zawadi Mauya.









