Yanga itakuwa mwenyeji wa miamba hiyo ya soka Misri na Afrika katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Soka Afrika.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm alisema amemaliza kazi kubwa kuwaanda wachezaji wake kisaikoloji.
Pluijm anaamini kuwa, maandalizi mazuri ya timu ni pamoja na kuwaanda wachezaji kisaikolojia, jambo analosema limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Alisema wachezaji wake wataingia dimbani kesho wakiwa na wanajiami kushinda mchezo huo na kusahau rekodi nzuri za timu za Uarabuni dhidi ya zile za Tanzania.
“Nachojivunia kwa sasa ni kwamba, wachezaji wangu wako kwenye hali nzuri na tayari kucheza dhidi ya timu bora Afrika,” alisema.
Alisema unapozifananisha timu hizo mbili kwa taswira ya nje, unaweza kusema Al Ahly zaidi ya Yanga, lakini wao hawana shaka na rekodi nzuri za mafanikio za timu hiyo Misri.
“Tuko tayari na mechi ya Jumamosi, tuko imara kila idara, nimewakumbusha wachezaji wangu kutokuwa na wasiwasi - mpira ni dakika 90,” alisema Pluijm.
Alisema amefurahi kurejea kwenye mazoezi kwa mshambuliaji wake, Simon Msuva aliyekuwa nje ya uwanja kutokana na kusumbuliwa na homa ya malaria.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema kuwa kambi yao ya Pemba imekuwa ya mafanikio na wanaamini watawashangaza Waarabu kwenye mchezo wao wa kesho.
”Tunashukuru kila kitu kimekwenda vizuri, kikubwa mashabiki wajitokeze kwa wingi kutushangilia,” alisema Mwambusi na kuongeza:
”Tunajua hila za Waarabu, wanakuja wakiwa na lengo la kupata goli la ugenini litakalowasaidia kwenye mchezo wa marudiano, hilo tumeliangalia na kuweka mikakati mizuri.”
Yanga inakutana na Al Ahly mara ya pili katika kipindi cha miaka miwili. Mwaka 2014 iliondolewa kwa matuta na 4-3 baada ya kila timu kushinda nyumbani kwake 1-0.
Imeandaliwa na Somoe Ng’tu na Faustine Feliciane










