Mshindi wa mechi hiyo anapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa licha ya timu zote mbili zitakuwa na mechi zingine 10 kabla kumalizika kwa msimu huu.
Licha ya Yanga kushinda mechi zote tatu walizokutana katika mechi za Ngao ya Jamii, mechi 15 zilizopita kati ya timu hizo Ligi Kuu zimeshindwa kumtoa mbabe, kila timu ikishinda mara tano na kutoka sare mara tano pia.
Lakini ubora wa vikosi vya pande zote mbili zinaifanya mechi ya leo kutotabirika kirahisi. Azam ambayo leo itakuwa mwenyeji wa Yanga, inashika nafasi ya pili nyuma ya Wanajangwani kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, wote wakiwa na pointi 46.
Kikosi cha Hans van der Pluijm kitaingia uwanjani kikiwa na kumbukumbu ya kukosa penalti katika mechi ya duru la kwanza waliyotoka sare ya 1-1, wakati Azam watahitaji kushinda au kulazisha sare ili kulinda rekodi yao nzuri ya kutopoteza dhidi ya Yanga Ligi Kuu tangu Februari 23, 2013 walipofungwa bao 1-0.
Nahodha wa Azam FC, John Bocco ambaye alitolewa kwa kadi nyekundu katika mechi yao iliyopita waliyotoka sare ya 1-1 katika hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu, amekuwa na rekodi nzuri ya kuitungua Yanga na leo ataongoza tena safu ya ushambuliaji akisaidiana na kinara wa mabao Azam FC, Kipre Tchetche.
Yanga ambayo inajivunia safu yake ya ushambuliaji iliyopewa jina la 'MTN' (Simon Msuva, Amissi Tambwe na Donald Ngoma) wanajivunia ukuta wa chuma ambao umeruhusu mabao tisa tu katika mechi 19 zilizopita za Ligi Kuu.
MTN kwa ujumla wamefunga mabao 32 Ligi Kuu msimu huu, Tambwe akitupia mara 15 akifuatwa na Ngoma (11) na Msuva (6), wakati Tchetche anaongoza kwenye kikosi cha Mwingereza Stewart Hall akiwa na magoli tisa akifuatwa na Bocco (8) na Shomari Kapombe (7).
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Majimaji watakuwa wageni wa African Sports, Toto Africans wakiikaribisha Ndanda FC jijini Mwanza, wakati Kagera Sugar wakiikabili Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
JKT Ruvu waliohamishia maskani yao kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, watawavaa Mwadui FC, Tanzania Prisons wakiwakaribisha Stand United mjini Mbeya huku mabingwa wa Tanzania Bara 1988, Coastal Union wakisafiri hadi Manungu kuchuana na mabingwa wa ligi hiyo 1999 na 2000, Mtibwa Sugar.
Simba itakuwa mwenyeji wa Mbeya City katika mechi pekee ya raundi ya 20 itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa kesho.










