Kipigo cha bao 1-0 walichopata kutoka West Brom Jumapili iliyopita kimepunguza kasi ya timu hiyo kumaliza msimamo na kushika moja ya nafasi nne za juu Ligi Kuu England.
Hiyo ina maana kwamba, kikosi hicho kiko kwenye hatari ya kushindwa kufuzu kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Lakini pia kipigo cha mabao 2-0 kutoka Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield katikati ya wiki hii kimepunguza nafasi pia ya kucheza michuano hiyo kupitia Ligi ya Europa.
United wana ratiba ngumu kwa sasa, watacheza na Liverpool katika mechi ya marudiano Ligi ya Europa hatua ya 16-bora, huku wakiwa nyuma kwa mbao 2-0, watakumbana pia na Manchester City wiki ijayo katika mchezo wa Ligi Kuu, kabla ya kucheza robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya West Ham Jumapili.
Mechi hizo zitakuwa kiini cha uamuzi wa ama kuendelea kubaki Old Trafford au kutimuliwa.
Pamoja na kocha huyo kutokuwa kwazi kuzungumzia mchezo wa Jumapili, lakini kuna dalili kubwa kwamba matokeo ya mechi za wiki inayofuata yataamua hatima yake.
"Nisingependa kulizungumzia hili kwenu kwa sababu ninyi siyo sehemu ya watu watakaofanya uamuzi juu yangu,'' alisema Van Gaal.
"Nafahamu, kipigo kutoka Liverpool kimetuacha kwenye wakati mgumu."Tuko kwenye mashindano makubwa matatu, baada ya kipigo dhidi ya Midtjylland mlishanifukuza kazi, lakini tulisimama, na sasa tuko raundi nyingine, inawezekana ikawa hivyo pia tutakapocheza na Liverpool.
Kuhusu mfumo anaotumia, Van Gaal alisema: “Mfumo unafanya kazi vizuri hata kama hautoi matokeo mazuri. Inapendeza muda wote unapofikiria kuwa bingwa, kushinda Ligi ya Europa au Kombe la FA.
"Hakuna kinachoshindikana, unapoangalia mechi yetu dhidi ya [Liverpool], mnaweza kusema mnachosema, lakini unapotakiwa kueleza mchanganua wa tuliyofanya msimu huu na msimu uliopita, hilo hamko tayari kueleza.
"Siwezi kuzibadilisha akili zenu kwa sababu tayari mna majibu, vinginevyo msiniulize maswali.''










