Waziri Chana apongeza jitihada Exim kuinua Golf Wanawake

24May 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waziri Chana apongeza jitihada Exim kuinua Golf Wanawake

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Balozi Dk. Pindi Chana amepongeza jitihada za Benki ya Exim Tanzania katika kudhamini matukio mbalimbali ya wanawake nchini ikiwemo michezo huku akibainisha nia ya Serikali ya kushirikiana na wadau mbalimbali nchini ili kuboresha hali ya michezo nchini ukiwemo

 

Dk. Chana ameibanisha nia hiyo ya serikali wakati akiongoza hafla fupi ya kuhitimisha mashindano ya wazi ya mchezo wa gofu ya wanawake ya 'Lugalo Ladies Open 2023' yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Klabu ya mchezo huo ya Lugalo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Mashindano hayo yaliratibiwa na Chama cha Golf cha Wanawake Tanzania (TLGU) na kufanyika kwenye viwanja vya Lugalo.

“Pamoja na kuipongeza Benki ya Exim Tanzania na wadau wengine waliojitokeza kufanikisha mashindano haya nitumie fursa hii kuwapa taarifa njema kwamba tayari Serikali imeanza kutekeleza jitihada kadhaa ili kuinua hali ya mchezo wa gofu nchini ikiwemo kukutana na wadau wa mchezo husika ili kujadili namna sahihi ya kuboresha mchezo huu pendwa,’’ alisema  Dk Chana.

Aidha, alisema Serikali inaangalia namna ya kuajiri mkufunzi wa kimataifa wa gofu nchini kufuatia ombi la wadau wa mchezo huo huku pia ikihakikisha nguvu zinazoelekezwa kwenye maboresho ya mchezo wa mpira wa miguu nchini zikielekezwa pia kwenye michezo mingine ukiwemo mchezo huo wa gofu.

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na wacheza gofu wa kike kutoka vilabu mbalimbali nchini, ilikua fursa kwa benki ya Exim Tanzania kutangaza bidhaa yake mpya ya Supa Woman inayolenga kusaidia wanawake kusimamia fedha zao kwa ufanisi na kufikia malengo yao ya binafsi na kitaaluma.

Kwa upande wake, Mkuu wa bidhaa za rejareja na uhakika wa mapato wa benki hiyo,  Mtenya Cheya, alisema kupitia bidhaa ya Supa Woman benki hiyo inajivunia kuunga mkono wanamichezo wa kike na kutambua mafanikio yao bora katika michezo .

" Tunatumai kuwa ushiriki wetu kwenye mashindano haya ya gofu utawatia moyo wanawake zaidi ili kufuata matamanio yao na kufikia malengo yao, ndani na nje ya uwanja wa gofu." alisema Mtenya.

Aidha Mwenyekiti wa Chama cha Gofu cha Wanawake nchini (TLGU) Queen Siraki alisema pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali kuendeleza michezo nchini pia alimuomba Waziri Chana kuwashawishi viongozi wakiwemo wabunge wanawake kushiriki kwenye mchezo huo ili kuongeza hamasa miongoni mwa wanawake nchini.