Hatua hiyo imefikiwa baada ya nyota hao kudaiwa kuihujumu timu kwenye mchezo wa 'Kariakoo Derby' dhidi ya Yanga na kusababisha kufungwa mabao 5-1, Novemba 5, mwaka huu, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Nipashe , Mtendaji Mkuu wa Simba, Iman Kajula, alisema Simba haifanyi jambo kwa kukurupuka na kila sehemu ina kamati mbalimbali ikiwamo uchunguzi na nidhamu.
Alisema katika fununu zilizotolewa kuhusu wachezaji hao, linafanyiwa kazi na kupelekwa kwenye kamati ya nidhamu ambayo inawajibu kufanyia kazi na kutoa hukumu pale ambapo kuna bainika kuna makosa.
“Zile fununu au tetesi za nyota hao tayari zinafanyiwa kazi na kamati itakuja kutolea majibu endapo itabainika kuna makosa, viongozi watatekeleza kwa kuchukuwa hatua," alisema Kajula.
Aliongeza: "Klabu ya Simba tunaamini kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya michezo lazima kuwapo nidhamu sifa ya kwanza kwa mchezaji uongozi hawatafumbia macho mchezaji au mwajiriwa ndani ya klabu hii anayeonesha utovu wa nidhamu."
Alisema lazima mchezaji au mwajiriwa ndani ya klabu hiyo atahukumiwa kulingana na jambo ambalo amelifanya pindi uchunguzi wa kina na kamati ya nidhamu zitakapojiridhisha.
Kuhusu mrithi wa Robertinho Oliveira, Kajula alisema mchakato unaendelea na siku chache zijazo watamtangaza kocha mkuu pamoja na wa viungo.
Alisema wamepokea CV nyingi za makocha mbalimbali lakini wameweka vigezo vyao na tayari amepatikana, hivyo kinachosubiriwa ni muda wa kumtambulisha rasmi.
“Ni kweli tunahitaji kupata kocha mkuu kabla ya haya mapumziko ya Kalenda ya Fifa kufikia tamati, tungependa wiki ijayo tunapokwenda kwenye mchezo wa kimataifa dhidi ya Asec Mimosas tuwe tayari tumeshamtangaza kocha wetu,” alisema Kajula.
Mtendaji huyo aliwataka mashabiki wa Simba kutulia na kuendelea kuunga mkono viongozi na wachezaji kuelekea maandalizi ya mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast .
“Makocha walikuwapo wanaendelea na majukumu yao ya kukisuka kikosi kwa wachezaji wetu kujiandaa na mchezo huo kusaka ushundi na kutafuta alama tatu muhimu za nyumbani,” alisema Mtendaji huyo.










