Washindi mbio za magari wapongezwa

01Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Washindi mbio za magari wapongezwa

BENKI ya Exim Tanzania imepongeza timu ya mbio za magari ya Hari Singh kufuatia ushindi iliyoupata hivi karibuni kwenye mbio za magari za Vaisakhi zilizofanyika mjini Moshi.

Timu hiyo inayodhaminiwa na Benki ya Exim Tanzania, imeweka rekodi ya kushinda mbio hizo kwa miaka mitatu mfululizo na inaundwa na dereva wa Kitanzania, Gurjit Singh Dhani na msaidizi wake, Shameer Yusuf.

Ilifanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye mbio hizo baada ya kutumia muda wa 01:23:36 kwa kutumia gari aina ya Subaru GVB2015.

Akitoa pongezi kwa niaba ya benki baada ya kumalizika kwa mbio hizo, Mwakilishi wa benki hiyo, Lameck Charles, alisema mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa yalichangiwa na uwezo mkubwa ulioonyeshwa na timu hiyo sambamba na uwezo mkubwa wa gari waliyoitumia.

“Exim kama wadhamini wa timu hii, tunachukulia ushindi huu kama mafanikio yetu pia na ni zawadi ya msimu wa Pasaka. Uwezo mkubwa wa timu hii ukichagizwa na udhamini wa Exim,’’ alisema Mwakilishi mwingine, Philip Mtei.

Akizungumzia ushindi huo, dereva Gurjit alisema pamoja na uwezo mkubwa wa timu yake, pia ulichagizwa na maandalizi mazuri, ubora wa gari pamoja na ushirikiano mzuri alioupata kutoka kwa wadhamini hao.

“Ushindani ulikuwa ni mkubwa na changamoto pia zilikuwapo ila mwisho wa siku tunashukuru sana kwa ushindi wetu,’’ alisema mshindi huyo.