Wafungwa jela maisha kujihusisha na soka

04Apr 2016
Nipashe
Wafungwa jela maisha kujihusisha na soka

TIMU ya Geita Gold Sport, JKT Oljoro na Polisi Tabora, zimeshushwa Ligi Daraja la Pili baada ya kutiwa hatiani kupanga matokeo ya mechi za Ligi Daraja la Kwanza Kundi C.

Kadhalika, Timu ya JKT Kanembwa nao wameshushwa daraja na sasa watacheza ligi ya mkoa.

Timu hizo zinadaiwa kupanga matokeo ya Ligi Dara la Kwanza kwa Geita kushinda mabao 8-0, huku Polisi Tabora wakitoka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya JKT Oljoro.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Jerome Msemwa alisema adhabu hiyo imetokana na kifungu 69 kinachofafanua adhabu ya mtu, timu na viongozi endapo watabainika kupanga matokeo ya timu.

Alisema kifungu hicho kimetumika kuzihukumu timu hizo pamoja na baadhi ya viongozi na wachezaji waliouhiska kupanga matokeo.

Wengine waliokubwa na adhabu hiyo ni mwamuzi aliyechezesha mechi ya Geita na Kanembwa, Saleh Mang'ola na Kamisaa Moshi Juma, ambao wamefungiwa maisha kujihusisha na soka.

Kadhalika, kocha msaidizi wa Geita Choki Abeid naye kafungiwa maisha, wakati kipa wa JKT Kanembwe Denis Richard amefungiwa miaka 10 na kutakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 10, huku kipa wa Geita naye amepigwa miaka 10 na faini ya Sh. milioni 10.

Wanafamilia wa soka wengine waliokumbwa na adha hiyo ni Katibu Mkuu wa chama cha soka mkoani, ambaye naye amefungiwa maisha, huku mwamuzi wa mechi ya Polisi Tabora na JKT Orjolo Masoud Mkelemi na Kamisaa Fedian Machunde wamefungiwa miaka 10 na kulipa faini Sh. 10 milioni.

Katibu wa Polisi Tabora, Alex Katenga hakupatikana na hatia, hivyo hakuwa miongoni mwa waliopea adhabu.
Kocha msaidizi wa Polisi Tabora, Bernard Fabian amefungiwa maisha kama ilivyo kwa mwenyekiti wa Oljoro, Amosi Mwita.