TFF yashtukia upangaji matokeo Championship

02May 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
TFF yashtukia upangaji matokeo Championship

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema linafuatilia kwa ukaribu suala la tuhuma za rushwa kwenye mechi ya Ligi ya Championship kati ya Fountain Gate FC na Kitayosce

 iliyochezwa Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa CCM Gairo, Morogoro na timu hizo kutoka suluhu.

Taarifa iliyotolewa na TFF kupitia kwa Afisa Habari na Mawasiliano wake, Cliford Ndimbo, imeeleza kuwa Sekretarieti ya TFF itafanya uchunguzi wa tukio hilo hadi dakika za mwisho na itachukua hatua kwa mujibu wa taratibu za mpira wa miguu.

Ni mechi ambayo imeendelea kuiweka Kitayosce yenye maskani yake mkoani Tabora, kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 54, ikipigana vikumbo na Pamba ya Mwanza iliyopo nyuma yao na alama zake 53.

Ligi hiyo iliendelea tena juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba wakati wenyeji Copco ilipoichapa Green Warriors mabao 2-1.

Ni matokeo ambayo yanaifanya Copco kufikisha pointi 23 ikiwa kwenye nafasi ya 11, huku Green Warriors ikiwa nafasi ya 13 na pointi zake 23 pia, lakini timu hizo zimeachana kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

TFF ilitangaza kuwa itakuwa makini kwenye mechi za mwisho ambazo kuna timu zinazowania kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara, huku JKT Tanzania ikiwa tayari imepanda, na zingine zikicheza kuepuka kushuka daraja.

Wakati Kitayosce na Pamba zikiwania kupanda Ligi Kuu, timu za Ndanda, Pan African, Green Warriors, African Sports na Copco zipo hatarini kushuka daraja kama hazitafanya vema kwenye mechi zao tatu zilizosalia.