TFF yalegea Uchaguzi Mkuu Yanga

08Jun 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
TFF yalegea Uchaguzi Mkuu Yanga

SARAKASI za utata wa kimamlaka kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa Yanga,

Rais wa TFF, Jamal Malinzi

Zilifikia tamati jana baada ya pande zilizokuwa zikisigishana kufikia suluhu na sasa uchaguzi huo utafanyika Jumamosi wiki hii kama klabu hiyo ya Jangwani ilivyotangaza awali na siyo Juni 25 kama ilivyoelezwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Uamuzi huo una maana kuwa, Yanga itafanya uchaguzi wake mkuu Juni 11 na siyo Juni 25 kama ilivyokuwa imetangazwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Awali, kulikuwa mvutano kikatiba kati ya Yanga na TFF, huku kila upande ukija na tarehe yake ya kufanyika kwa uchaguzi huo na pia kila upande ukitaka kubeba mamlaka ya usimamizi.

Katika kikao hicho kilichofanyika jana chini ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na kuwashirikisha Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga na katibu wake, Baraka Deusdetit, kiliamua uchaguzi wa Yanga kufanyika kwa tarehe iliyopangwa na klabu hiyo na siyo kinyume chake.

Kadhalika, kikao hicho kilimaliza mgongano wa kamati gani ina haki ya kusimamia uchaguzi huo, ambapo sasa TFF kupitia kamati yake ya uchaguzi ndiyo itakayobeba jukumu la kusimamia.

Kabla ya uamuzi huo, Yanga ilikataa uchaguzi huo kusimamiwa na Kamati ya TFF, badala yake walitaka usimamiwe na kamati yao wenyewe.

Serikali iliingilia kati uchaguzi wa klabu hiyo kupitia Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kwa kuitaka kuitisha uchaguzi baada ya muda mrefu wa bila kuchagua viongozi wapya kama katiba inavyoelekeza.

Hata hivyo, uamuzi wa TFF kuingilia kati mchakato wa uchaguzi wa Yanga, ulizua kasheshe kubwa, huku Yanga ikidai inahujumiwa na vigogo wa TFF na BMT.

Kutoka na mtafaruku huo, juzi klabu hiyo iliamua kupeleka malalamiko Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ikidai kuna harufu ya rushwa yenye lengo la kuleta hujuma.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema jana kuwa, kikao cha vigogo hao kilikubaliana kuwa wanachama wote waliokuwa wamechukua fomu za uchaguzi kwenye ofisi za TFF kujumuishwa kwenye mchakato wa uchaguzi huo.

Awali, uongozi wa Yanga ulitangaza kuwasimamisha uanachama wanachama saba wa klabu hiyo waliochukua fomu TFF.

"Kikao kimeamua wote waliokuwa wamechukua fomu hapa TFF na uongozi wa Yanga kuwasimamisha, wajumuishwe kwenye uchaguzi huo," alisema Lucas.

Tayari wanachama 19 walipitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kuwania uongozi kwenye uchaguzi huo baada ya kukata majina ya wanachama wawili ambao hawakuwa na sifa.

Kurejeshwa kwa wanachama waliokuwa wamechukua fomu TFF, kunafanya uchaguzi huo kuwa na wagombea 26 hadi sasa.