Straika wa Fountain Gate Princess aula kama Opa

27Mar 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Straika wa Fountain Gate Princess aula kama Opa

SIKU chache baada ya straika wa Simba Queens, Opa Clement, kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa nchini Uturuki katika Klabu ya Besiktas, mchezaji mwingine anayechezea Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, Cynthia Musungu,

Raia wa Kenya naye amekwenda nchini humo kujiunga na timu hiyo.

Taarifa zilizotolewa na Klabu ya Fountain Gate Princess, ambayo kwa sasa inaongoza Ligi Kuu ya Wanawake kwa pointi 29, Musungu ambaye naye pia alikuwa na mabao tisa kama Opa, zimeeleza amekwenda kujiunga na Klabu ya Besiktas.

Klabu hiyo imemtakia kila la kheri mchezaji wao huyo kwenye maisha yake mapya ya soka na timu yake hiyo mpya.

Musungu amekuwa tegemeo kwa kikosi cha Foutain Gate Princess na kwa kiasi kikubwa mabao yake ndiyo yaliyofanya timu hiyo kuwa kileleni.

Huu ni mfululizo wa wachezaji wanaocheza soka nchini, hasa Ligi Kuu ya Tanzania kwa wanawake kununuliwa na kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Machi mwaka jana Opa, alikwenda Klabu ya Kayserispor Girl ya Uturuki kwa kile kilichoelezwa ni kufanya majaribio na akifanikiwa klabu hiyo ingekaa mezani na Simba kumalizaka, lakini alirejea nchini na baadaye haikufahamika kama alifuzu au la.

Hata hivyo, Klabu ya Besiktas mwaka huu ilikuja kumchukua moja kwa moja baada ya kuridhika na kiwango chake ambacho walikiona akikionyesha kwenye klabu nyingine aliyokwenda kufanyia majaribio.

 Machi 2021, Simba Queens pia ilimuuza aliyekuwa nahodha wake wakati huo, Mwanahamisi Omari kwa klabu ya Shabab Atlas ya Morocco, lakini kwa sasa amerejea tena klabu ya Msimabazi kwenye kipindi cha dirisha dogo la usajili na anaendelea kucheza Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania akisikilizia dili lingine kama litakuja.

Mchezaji mwingine ni kiungo Flavian Mawete Musolo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo aliyeichezea Simba Queens mwaka 2020 hadi 2021, ambapo aliuzwa kwa Klabu ya Adana Idmanyurduspor ya Uturuki anayoichezea hadi sasa.