Stars yafufua matumaini kutinga AFCON

20Jun 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Stars yafufua matumaini kutinga AFCON

BAO pekee lililofungwa na mchezaji wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Al Qadsiah ya Saudi Arabia, Simon Msuva, jana liliifanya timu ya taifa,

Taifa Stars kufufua matumaini ya kukata tiketi, kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), zinazotarajiwa kufanyika mwakani Ivory Coast kwa kuifunga Niger bao 1-0.

Winga huyo alipachika bao hilo dakika ya 69, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na kiungo Novatus Dismas, anayecheza soka la kulipwa Ubelgiji kwenye klabu ya Zulte Waregem.

Faulo iliyopigwa na Dickson Job winga ya kulia, ilikatisha hadi winga ya kushoto, kiungo huyo akauchukua mpira na kuwazidi nguvu na maarifa mabeki wa Niger kabla ya kupiga krosi iliyounganishwa na Msuva, akiiwezesha Tanzania kupata ushindi wa kwanza nyumbani, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwenye mechi hiyo ya Kundi F, ya kusaka tiketi ya kucheza fainali hizo zinazotarajia kuanzia Januari 13 mwakani, hadi Februari 11, Stars ilitawala zaidi kipindi cha kwanza, hasa dakika 20 za mwanzo na Niger ilitawala kipindi cha pili hasa dakika 15 za mwisho.

Sekunde ya 30 tu, Kibu Denis alimtoka Najeeb Yakoub na kupiga krosi iliyowababatiza mabeki wa Niger na kuwa kona ambayo ilienda kupigwa na Mudathir Yahaya na kuunganishwa vema na Simon Msuva, lakini ukatoka kidogo nje ya lango.

Stars iliendelea kulisakama lango la wapinzani wao, dakika ya nne ya mchezo, Mudathir Yahaya, akiwa umbali wa mita zipatazo 35, aliachia kombora kali ambalo kipa Djibrilla Kassali Djibo alitaka kuudaka, lakini ukamtoka na kwa bahati nzuri akauwahi tena.

Niger ilijibu shambulizi dakika ya tano, wakati beki wa kulia, Najeeb alipopanda mbele na kupiga krosi iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na wachezaji wenzake, lakini kwa bahati mbaya, ukatoka juu kidogo la lango.

Kibu, aliyekuwa kwenye kiwango kizuri kwenye mechi ya jana na kumsumbua mno beki wa kulia Najeeb, alifanya kazi ya ziada alipowatoka mabeki wa Niger dakika ya 12, na kumpa pasi Dickson Job ambaye alimimina majaro iliyokuwa ikisubiriwa na Mbwana Samatta, lakini kabla haujatua kichwani kwake, mabeki wa Niger waliuwahi na kuutoa kona, huku Kocha Mkuu wa Stars akiwa ameshasimama kutaka kushangilia bao.

Dakika nne baadaye, Msuva aliupata mpira kirahisi baada ya beki mmoja wa Niger kuanguka chini peke yake, akapiga krosi iliyounganishwa na Kibu, isivyo bahati, ukatoka kidogo tu pembeni ya lango la wapinzani.

Baada ya dakika 20 kupita, kasi ya Stars ilionekana kupungua na Niger kuanza kutawala pambano ikipiga pasi fupi fupi.

 

Moja kati ya shambulizi kali lililofanywa ni lile la dakika ya 38, wakati mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo, Daniel Sosah alipowazidi maarifa mabeki Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Abdallah 'Bacca' na hapo hapo, kipa Beno Kakolanya akiwa ametoka langoni.

Mshambuliaji huyo aliudokoa mpira na ukawa unaelekea wavuni, lakini kwa bahati haukuwa na kasi hivyo uliwahiwa na Kakolanya na kuinusuru Stars.

Kipindi cha pili Stars ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Kibu, Mudathir, na Msuva na nafasi zao kuchukuliwa na Muzamir Yassin, Tiba John na Himd Mao, mabadiliko ambayo hayakuisaidia sana Stars, badala yake iliruhusu sana mashambulizi na kama wachezaji wa Niger wangekuwa makini wangeweza kusawazisha au kushinda.

Winga Victorien Adebayor aliyeingia dakika tano kabla ya mechi kumalika, nusura afunge mabao dakika ya 86 na 90, na Abdoulaye Karim Doudou naye akikosa baada ya kupiga juu akiwa kwenye nafasi nzuri ya kusawazisha.

Kwa ushindi huo, Stars imefikisha jumla ya pointi saba nyuma ya Algeria, ambapo mechi ya Uganda dhidi ya Algeria ilikuwa ikiendelea usiku jana jioni kwenye uwanja wa Japoma nchini Cameroon hadi hadi tunakwenda mitamboni timu hizo zilikuwa hazijafungana.

Uganda inacheza mechi zake nje ya nchi kutokana viwanja vyao kutokidhi vigezo vilivyowekwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).