Klabu hiyo imesema imeingia mkataba wa miaka miwili na kipa huyo ambaye tayari ameungana na makipa wengine waliopo kambini nchini Uturuki, Ally Salim na Ahmed Feruzi Telu, kwa maandalizi ya mashindano ya msimu ujao, huku ikiendelea kumsubiria kipa mwingine Aishi Manula ambaye aliumia mwishoni mwa msimu uliopita na kufanyiwa operesheni itakayomweka nje zaidi ya miezi mitatu.
"Tumefanikiwa kumpata golikipa Jefferson Luis, karibu sana. Tayari mlinda mlango huyo ameungana na kikosi nchini Uturuki kuendelea na mazoezi ya maandalizi ya msimu wa mashindano 2023/24 akitokea Brazil," ilieleza taarifa ya Simba na kuongeza.
"Jefferson ana uwezo mkubwa wa kulinda lango huku akitumia miguu yote miwili kwa ufasaha na kumudu kuanzisha mashambulizi pia akiwa na uzoefu wa kucheza mechi nyingi za ushindani."
Kipa huyo mwenye uzito wa kilo 84 na urefu wa sentimeta 192 (mita 1.92), anaonekana kuja kuleta chachu kwenye eneo la golikipa ambalo tangu mwaka 2017, lilikuwa chini ya himaya ya Manula.
Hata hivyo, hakuna shabiki yeyote wa soka nchini wakiwamo wanachama na wapenzi wa Simba waliotegemea kusajiliwa kipa huyu, badala yake wengi walidhani atakuwa mmoja wa wale wawili ambao walitajwa sana kwenye tetesi, akiwamo Mbrazil Caique Luiz Santos na Simon Omossola raia wa Cameroon anayeichezea FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Awali, taarifa za ndani ya klabu zilibainisha kuwa Simba waliachana na Mbazil Caique kwa sababu hajui lugha ya Kingereza wala Kifaransa, badala yake anafahamu Kireno kitu ambacho kiliwafanya mabosi wa klabu kuwa na wasiwasi jinsi atakavyokuwa akiwasiliana na mabeki wa timu hiyo wanaofahamu zaidi lugha za Kifaransa, Kiingereza na Kiswahili.
Taarifa zilizidi kudai kuwa viongozi wa Simba waliangukia kwa Omossola na tayari walishaanza mazungumzo, lakini Kocha Mkuu, Mbazili Robertinho Oliveira, alikatisha dili hilo kwani aliwaambia anataka kipa kutoka Brazil na si vinginevyo.
"Alituambia anataka kipa kutoka Brazil tu kwa gharama yoyote ile, kwa hiyo ikaanza kazi nyingine ya kumsaka kipa bora na ambaye atafahamu angalau lugha ya Kiingereza, tumempata huyu kwa msaada wake pia, ni kipa mzuri sana," kilisema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.
Kusajiliwa kwa kipa huyo na Luis Miquissone kunafanya timu hiyo kuwa na wachezaji 14 wa kigeni, hivyo ni lazima wawili wakatwe ili kukidhi kanuni ya Ligi Kuu Bara.
Lakini Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema wanachofanya kwanza ni kusajili kila mchezaji ambaye wanamhitaji na baadaye ndipo watakaa kuangalia nani ampishe nani.









