Simba, Yanga zinachanga karata

15Apr 2023
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba, Yanga zinachanga karata
  • ***Makocha waendeleza tambo, umakini na kutobweteka silaha muhimu...

MUDA utazungumza, ndicho kilichobakia kuelekea mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga itakayochezwa kesho kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Makocha wa timu hizo, kila mmoja ametamba kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka ndani na nje ya Tanzania.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, alisema jana wanajua mechi hiyo itakuwa ngumu, lakini watacheza kama fainali kwa ajili ya kuusaka ushindi na kujiimarisha kwenye mbio za kutetea ubingwa wanaoushikilia.

Kaze alisema wameisubiri sana mechi hiyo ya dabi na wao kama vinara wa ligi wanahitaji pointi tatu na si matokeo mengine licha ya kutambua mchezo huo utakuwa na ushindani unaotokana na ubora wa wapinzani wao.

Kocha huyo alisema wanajiandaa kufanya mabadiliko katika sehemu kubwa ya kikosi chao hasa kwenye safu ya ulinzi na hii inatokana na kuimarika kwa Simba katika siku za hivi karibuni.

" Tunafanya mazoezi kulingana na aina ya mechi tunaenda kucheza, tumekuwa na timu ambayo imekuwa inabadilika kila wakati, mabadiliko yatakuwapo katika maeneo mengi ikiwamo safu ya ulinzi ingawa siyo sasa naweza kutaja nani atakuwapo," alisema Kaze.

Aliongeza wataongeza umakini katika mechi hiyo itakayotoa mwanga wa mbio za ubingwa wa msimu huu lakini pia kujiweka imara kuelekea mechi yao ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Alisema pia hawataingia kwa kubweteka na rekodi, kwa sababu siku zote 'dabi' huwa haitabiriki.

"Ni mechi ambayo inasubiriwa na mashabiki wengi, tunajua nini cha kufanya, dabi siku zote haitabiriki, anayekuja kwa kupambana na kujituma, kufuata vizuri maelekezo ya walimu ndiyo anashinda, kuongoza kwetu ligi na nafasi tuliyonayo haitupi au kutusaidia lolote kupata ushindi, kitu kikubwa ni kujituma na kucheza kama fainali, hilo tunalijua na tupo tayari," Kaze alisema.

Naye Juma Mgunda alisema Simba imejipanga kucheza mechi hiyo kama fainali kwa sababu ndio utakaoamua hatima ya mbio za ubingwa kwa upande wao.

Mgunda alisema kikosi chao kilianza mazoezi mara baada ya kumaliza mechi dhidi ya Ihefu kwa sababu walifahamu wanahitaji kuwa imara zaidi katika kila eneo.

"Siyo kama tulianza maandalizi juzi, tulikuwa tunaijua, na tarehe inafahamika kwa hiyo mechi hii tumejiandaa muda mrefu tu, hiki unachokiona ni tunakamilisha tu maandalizi ya mwisho ya mchezo. Tunaweza kusema mchezo ni mzito, tunaweza kusema una hatima yetu.

Vile vile kwa sababu bado tuko kwenye mbio za ubingwa na mimi huwa kila siku nasema 'haiwi mwisho hadi iwe mwisho', bingwa atapatikana baada ya ligi kumalizika. Tunaichukulia mechi hii kwa umuhimu wa kipekee kabisa," alisema Mgunda ambaye ndiye mwenyeji wa mechi hiyo.

Katika mechi hiyo, Yanga inajivunia ubora wa wachezaji wake wakiongozwa na  Stephane Aziz Ki aliyefunga bao la kusawazisha kwenye mechi iliyopita, Fiston Mayele, straika tegemeo wa kikosi hicho, lakini pia wapo mawinga hatari kama Jesus Moloko na Tuisila Kisinda huku idara ya ulinzi ikiongozwa na Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Djuma Shaaban.

Simba yenyewe itashuka katika dabi hiyo ikimtumia kwa mara ya kwanza ni Jean Baleke, straika wa kumainiwa kwa sasa na timu hiyo, Saido Ntibazonkiza ambaye ameshawahi kucheza dabi, lakini itakuwa ni ya kwanza akiwa na Wekundu wa Msimbazi pamoja na nyota, Clatous Chama, Pape Sakho na Kibu Denis.

 

Imeandikwa na Adam Fungamwango na Saada Akida