Simba ilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi iliyopita kwa kuirarua Horoya ya Guinea mabao 7-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku Yanga ikifanya hivyo Jumapili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuichapa US Monastir ya Tunisia mabao 2-0.
Timu zote mbili zimefanikiwa kutinga hatua hiyo zikiwa na mchezo mmoja mkononi wa ugenini, Simba ikitarajiwa kumaliza dhidi ya Raja Casablanca nchini Morocco wakati Yanga ikimaliza dhidi ya TP Mazembe nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na Mwenyekiti wa Wanachama wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, wamesema timu zao zinaweza kuvuka hatua hii endapo wakiendelea kupambana kama walivyofanya kwenye hatua za makundi.
"Mpira si jambo la kuelezewa sana zaidi ya vitendo, walio uwanjani wameona na kwenye televisheni wameona na waliokuwa kwenye redio wamesikia, timu imecheza mpira kwenye kiwango kizuri na tumepata ushindi, hakuna kingine, timu si ya mtu au mchezaji mmoja, kila mmoja amecheza kwa nafasi yake na kiwango chake, jambo kubwa ambalo ninalolisema tunawapongeza wachezaji wote kwa kutekeleza mipango au 'plani' ya kocha na ikafanikiwa.
"Tunakwenda kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Raja Casablaca kwa ajili ya kupata matokeo mazuri pamoja na kwamba tumeshavuka hatua hii, lakini tutakwenda kuleta ushindani kwa sababu mpira si ushindi peke yake ila pia ni burudani kwa hiyo lazima tuwaburudishe Waafrika na watu wengine duniani ambao watakuwa wanaangalia mchezo huu, kwa hiyo wachezaji wetu watatakiwa kuwaonyesha kile kilichosababisha wafike hapo walipo na nina uhakika tukiendelea kuweka nguvu tunaweza kusonga mbele zaidi kwenye hatua hii tuliyofikia," alisema Mangungu.
Naye Injinia Hersi alisema Taifa limepata heshima kuwa na timu mbili za Tanzania kuingia kwa pamoja kwenye michuano ya kimataifa na kuiona ikichanja mbuga.
Aidha, aliihakikishia serikali, wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa timu hiyo haitoishia njiani kwani waliweka malengo ya kufanikiwa kwenye mashindano ya ndani na wamefanya hivyo na sasa wanaweka malengo ya kufanikiwa kimataifa na hawatoliangusha taifa.
"Nawashukuru sana Wanayanga kwa nguvu walioionyesha mpaka leo tumeweza kupata haya matokeo, safari bado haijaisha, tulikuwa na malengo, tulikuwa na malengo ya kuvuka makundi, tumevuka sasa leo tumeingia robo fainali waendelee kutusapoti, huwezi kujua, inaweza kuwa nusu fainali, fainali au ubingwa," alisema Hersi.










