Simba , Yanga kazi iendelee

30Mar 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba , Yanga kazi iendelee
  • Makocha watamba wanafuata ushindi kwa ajili ya kujiimarisha kuelekea...

WAKATI kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka nchini leo kuelekea Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kuwafuata TP Mazembe, kundi la kwanza la Wekundu wa Msimbazi limewasili Morocco tayari kuwakabili wenyeji Raja Casablanca.

 

Hata hivyo kikosi cha Simba kilichokuwa na wachezaji 13, benchi la ufundi na viongozi juzi kilikwama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mkoa wa Kilimanjaro (KIA), baada ya ndege waliokuwa wakisafiria kupata hitilafu na hivyo walilazimika kulala jijini, Arusha.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema ndege waliyokuwa wakisafiria ilipata hitilafu na walitaarifiwa safari haitaendelea.

Kundi la pili la wachezaji wa timu hiyo ambayo walikuwa katika majukumu ya kimataifa lilitarajiwa kuwasili Morocco kwa nyakati tofauti leo kwa ajili ya mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kwenye Uwanja wa Momamed V usiku wa kuamkia Jumamosi.

Vinara wa Kundi C, Raja Casablanda yenye pointi 13 na Simba inayofuata yenye pointi tisa, zimeshasonga mbele katika michuano hiyo.

Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' amesema pamoja na kutinga  robo fainali, lakini wanakwenda kupambana kwa ajili ya kusaka ushindi na kukiweka sawa kikosi chake kuelekea hatua inayofuata.

"Tuko katika kiwango kizuri sasa kuliko mwanzo tulipokutana nao, hivi sasa wachezaji wangu wapo moto, kuna Kibu Denis, kuna kiwango bora cha Jean Baleke, halafu nyuma hapa nina, Clatous Chama na Saido Ntobazonkiza, wote wapo kwenye kiwango cha juu kuliko mwanzo tulipokutana nao, tunaweza kabisa kulipa kisasi, " alisema Robertino.

Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameliambia gazeti hili yuko tayari kukutana na timu yoyote katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika na sasa wanaenda kusaka ushindi ili kumaliza kileleni katika kundi lao.

Kocha huyo alisema wana kazi kubwa ya kufanya katika mechi yao dhidi ya TP Mazembe lakini hawana hofu kutokana na uimara wa wachezaji wake kwa sasa.

Alisema kazi kubwa anayoifanya ni kuwasisitiza wachezaji wake kuongeza umakini wa kutumia vyema nafasi wanazotengeneza na hiyo itawasaidia katika mechi muhimu ya hatua ya robo fainali.

“Ni kweli tayari tumetinga robo fainali huku tukiwa na mechi moja mkononi dhidi ya TP Mazembe, mchezo utakuwa mgumu, tunahitaji kupata pointi tatu ili tuongoze kundi, lakini tuko tayari kukutana na timu yoyote ambayo tutapangwa nayo katika hatua inayofuata ya robo fainali,” alisema Nabi.

Aliongeza hatua waliyofika ni ngumu zaidi na mechi dhidi ya TP Mazembe ni muhimu ili kuwaandaa wachezaji wake na hatua ya mtoano ambayo wanaelekea.

"Tunakwenda kutafuta matokeo chanya licha ya kutambua mchezo huo utakuwa mgumu, washambuliaji wanatakiwa kuwa makini na kuhakikisha hawapotezi nafasi wanazotengeneza ili kutafuta ushindi, kila mchezaji anatakiwa kujiimarisha na kutumia mechi hii kujiweka tayari na vita iliyoko mbele yetu," aliongeza kocha huyo.

Aliongeza wachezaji wote waliokuwa katika kikosi cha Timu ya Tanzania (Taifa Stars), wamesharejea kambini isipokuwa kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambaye bado ameendelea na msimamo wake wa kutohitaji kurejea ndani ya timu hiyo.