Safu ya ushambuliaji ya Simba inaongozwa na Jean Baleke, Moses Phiri na John Bocco ambaye alikosa nafasi nyingi za wazi katika mchezo uliopita.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa simu, Mgunda alisema wameona madhaifu ya kikosi chao hasa safu yao ya ushambuliaji kwa kutokuwa makini na kukosa utulivu hivyo kuandaa programu maalum katika mazoezi.
Alisema katika programu hiyo ni pamoja na kuwajenga kisaikolojia wachezaji wao na anaimani kubwa ya kufanya vizuri katika michezo iliyosalia ukiwamo watakaocheza nyumbani dhidi ya Raja Casablanca Jumamosi.
“Ni mechi ngumu na ushindani mkubwa, ukizingatia tumetoka kupoteza, lakini tutakuwa nyumbani na tunahitaji kupata matokeo mazuri katika mchezo huo dhidi ya Raja Casablanca.
"Kwa washambuliaji wetu inawalazimu kuwa na umakini na utulivu kichwani ili kufikia malengo ya kukusanya pointi tatu kila mechi tutakayocheza nyumbani,” alisema Mgunda.
Alisema wamewasoma wapinzani wao katika mchezo uliopita walipocheza na Vipers ya Uganda katika mechi ya kwanza, kwa kuona ubora na madhaifu ya Raja Casablanca.
“Ni timu nzuri, lakini tunatarajia kupata matokeo mazuri katika ardhi ya nyumbani, ninaimani wachezaji wetu wako vizuri na tunaendelea na maandalizi katika mchezo wetu huo,” alisema Mgunda.
Simba wanarejea nchini leo na kuingia kambini moja kambini kujiandaa na mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya ligi hiyo dhidi ya Raja Casablanca utakaocheza Februari 18, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.










