Simba wana kazi kwa Singida Taifa leo

28Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Simba wana kazi kwa Singida Taifa leo

MICHUANO ya Kombe ka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation inatarajiwa kuendelea leo kwa michezo miwili ya hatua ya 16 Bora.

Timu ya Singida United

Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mabingwa wa mwaka 2000 wa Kombe hilo, Simba SC watakuwa wenyeji wa Singida United ya Singida, wakati Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wenyeji Toto African wataikaribisha Geita Gold ya Geita.

Singida inachagizwa na mafanikio ya kupandea Daraja la Kwanza kutoka la Pili wiki iliyopita, wakati Simba ina hasira ya kipigo cha 2-0 kutoka kwa mahasimu, Yanga wiki iliyopita.

Mechi za 16 Bora ya michuano hiyo, zitahitimishwa kesho kwa mchezo mmoja, kati ya wenyeji Panone FC dhidi ya Azam FC ya Dar es Salaam Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Timu zilizofanikiwa kuingia Robo Fainali za michuano hiyo hadi sasa ni Yanga iliyoitoa JKT Mlale kwa kuifunga 2-1 Februari 24, Ndanda FC iliyowatoa waliokuwa wanashikilia taji, JKT Ruvu kwa kuwafunga 3-0 na Coastal Union iliyoifunga 1-0 Mtibwa Sugar juzi, wakati mechi mbili zilichezwa jana kati ya Mwadui FC dhidi ya Rhino Rangers na Prisons dhidi ya Mbeya City.

MATOKEO NA RATIBA 16 BORA KOMBE LA TFF

Februari 24, 2016

Yanga SC 2-1 JKT Mlale (Taifa, Dar es Salaam)

Februari 26, 2016

Ndanda FC 3-0 JKT Ruvu (Nangwanda, Mtwara)

Coastal Union 1-0 Mtibwa Sugar (Mkwakwani, Tanga)

Februari 27, 2016

Mwadui FC Vs Rhino Rangers (Mwadui, Shinyanga)

Prisons Vs Mbeya City (Sokoine, Mbeya)

Leo; Februari 28, 2016

Simba SC Vs Singida United (Taifa, Dar es Salaam)

Toto African Vs Geita Gold (Kirumba, Mwanza)

Februari 29, 2016

Panone FC Vs Azam FC (Ushirika, Moshi)