Wakati Simba ikipata ushindi wa nne mfululizo chini ya kocha mkuu wa muda, Mganda Jackson Mayanja ilipoifumua
Licha ya matokeo hayo ambayo ni mwendelezo wa mwendo wa kusuasua baada ya Jumamosi kufungwa mabao 2-0 jijini Tanga dhidi ya Cosatal Union, Yanga bado wako kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 40 baada ya mechi 17, pointi moja nyuma ya Simba walioko nafasi ya pili wakiing'oa Azam FC kwa tofauti ya mabao.
Kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Yanga ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji Amissi Tambwe aliyemalizia kwa kichwa krosi iliyotua ndani ya sita kutoka kwenye mguu wa kushoto wa Haruna Niyonzima aliyecheza mechi yake ya kwanza jana baada ya kukosa mechi 12 zilizopita za mshindano (7 za Ligi Kuu).
Lilikuwa ni goli la 14 msimu huu kwa mfungaji bora huyo wa msimu wa 2013/14 aliokuwa na kikosi cha Simba.
Dakika tano baadaye, Prisons walisawazisha goli hilo kupitia kwa straika wao hatari Jeremiah Juma aliyejitwisha kichwa mpira wa krosi ya Mohamed Mkopi kutoka wingi ya kulia kusini mwa uwanja na kuzifanya timu hizo zipumzike zikiwa sare ya 1-1 huku akiandika goli lake la 10 msimu huu (sawa na namba ya jezi yake).
Dakika mbili baada ya saa ya mchezo, Mkopi aliipatia Prisons goli la pili akiuparaza kwa kichwa mpira wa faulo kali ya mguu wa kushoto wa mtokea benchini Juma Seif 'Kijiko' iliyotua ndani ya boksi kutoka wingi ya kulia kaskazini mwa uwanja huo.
Lilikuwa goli la tano kwa straika huyo aliyetupia pia katika ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Sokoine Oktoba 21 na la nne kwa kipa Deogratius Munishi 'Dida' kufungwa msimu huu. Kipa huyo alifungwa kwa mara ya kwanza katika kipigo cha 2-0 dhidi ya Coastal Jumamosi baada ya kucheza mechi saba bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Penalti ya dakika ya 85 iliyopigwa kwa mguu wa kulia na Msuva, ilizaa goli la pili la Yanga baada ya Benjamin Asukile kuushika mpira ndani ya boksi wakati akijaribu kuosha shuti la faulo iliyopigwa na Niyonzima. Lilikuwa ni goli la nne msimu huu kwa mfungaji bora huyo wa msimu uliopita.
Kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Hamis Kiiza alifunga goli lake la 13 msimu huu akimalizia kwa shuti la mguu wa kulia krosi ya mshambuliaji Ibrahim Ajibu ambaye aligongeana vizuri na beki wa pembeni Hassan Kessy katika dakika ya tano.
Dakika moja kabla ya robo saa ya mchezo, Mganda alipata nafasi ya kumpiku Tambwe kwa magoli, lakini akapiga penalti ya kichoyu iliyofutwa na kipa Mudathir Khamis na kuandika rekodi ya kuwa tuta la kwanza Simba kukosa msimu huu.
Penalti hiyo ya pili Simba kupewa msimu huu ilitolewa na refa Emmanuel Mwandembwa kutoka Arusha baada ya Henry Chacha kuunawa mpira wa shuti la Mganda huyo ndani ya boksi la Mgambo.
Dakika mbili kabla ya nusu saa ya mchezo, Simba walipata goli la pili lililofungwa na kiungo mzoefu Mwinyi Kazimoto aliyefumua shuti kali la mguu wa kulia nje ya boksi akiitendea haki kazi nzuri ya Ajibu.
Baada ya kuhusika katika upatikanaji wa mabao mawili ya awali, Ajibu alitupia goli la tatu la Simba dakika tatu kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza akimalizia pasi ya kiungo Jonas Mkude kwa kupiga shuti kali la kimo cha mbuzi ndani ya boksi na kuandikisha goli lake la saba msimu huu.
Akitoka benchi katika dakika ya 72 kuchukua nafasi ya Ajibu, mshambuliaji wa usajili wa dirisha dogo, Danny Lyanga alitumia dakika tano tu kupata goli lake la tatu msimu huu na la nne kwa Simba jana akiitendea haki pasi ya kiungo mtokea benchini Said Ndemla.
Katika dakika ya 82 Kiiza alimkamata Tambwe kwa kufikisha mabao 14 akiifungia Simba goli la tano na la 32 msimu huu kwa shuti la mguu wa kulia baada ya kupenyezewa pasi murua na beki wa pembeni kulia, Kessy.
Kiungo Fully Maganga alihakikisha kikosi cha Bakari Shime hakitoki kapa kwenye Uwanja wa Taifa akifunga goli la kufutia machozi dakika mbili kabla ya kipenga cha mwisho na kuweka rekodi ya goli la kwanza kwa timu hiyo kwenye Uwanja wa Taifa huku akifuta ndoto za Simba kucheza mechi tano (nne kwa kocha Mayanja) mfululizo bila kuruhusu nyao zao kutikiswa.
Mara ya mwisho kikosi cha Mganda huyo aliyerithi mikoba ya Muingereza Dylan Kerr, kuruhusu bao Ligi Kuu ilikuwa Desemba 26 mwaka jana walipotoka sare ya 1-1 dhidi ya Mwadui FC mjini Shinyanga.
MATOKEO MENGINE
Mtibwa 2-2 Toto
Imeandikwa na Nebart Msokwa (Mbeya, Somoe Ng'itu na Sanula Athanas (Dar)









