Simba itawakaribisha mabingwa watetezi, Wydad katika mechi ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa Tawi la Wekundu wa Chalinze, Pwani, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema baada ya miaka 20, imefika wakati timu yao ikaweka rekodi nyingine ya kuwavua ubingwa Wydad kama walivyofanya mwaka 2003.
"Tuna shughuli moja tu ya kwenda kumnyoa Wydad Casablaca ili tuandike historia nyingine ya kumvua mtu ubingwa. Tunajua mechi ni ngumu, tunacheza na mtu aliyetudizi viwango vya CAF, tunacheza na mabingwa watetezi, lakini Wanasimba tukiunganisha nguvu na kushikamana, Wydad Casablaca hawana pa kutokea.
Inaonekana ni kama ndoto ya mchana hivi tukizungumzia kuifunga, siku zote sisi tunazungumza kile ambacho tunachokiweza kwa sababu tumeshawahi kufanya hivyo huko nyuma," alisema Ahmed.
Aliongeza hata mwaka 2003 hakuna aliyeamini kama Simba inaweza kuwafunga Zamalek, na hata iliposhinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), watu hawakuamini kama wanakwenda kupata matokeo mazuri ugenini, badala yake kila mmoja alidhani itafungwa mabao mengi.
"Tumeshawahi kufanya hivyo, kwa hiyo tunazungumza tunachokiweza, tulipangiwa Zamalek, wakiwa wa moto kweli kweli lakini tukasimama imara tukamfunga kwenye Uwanja wa Uhuru, tukaenda kumtoa kwao, heshima ya mnyama, ikaandikwa Afrika. Miaka mingi imepita sasa, bado tuna heshima ya 2003, lakini muda umefika ya kuandika heshima mpya, nayo ni kumtoa Wydad Casablanca na kwenda nusu fainali, Wanasimba wote wanaamini inawezekana," alisema Ahmed.
Wydad Casablanca imetua na msafara wa watu zaidi ya 50, ambao ni wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na baadhi ya mashabiki.
Beki wa kati ya timu hiyo ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Arsene Zola, mara baada ya kuwasili alisema wamekuja kupambana kupata matokeo mazuri kwa ajili ya kurahisisha kazi kuelekea mechi ya marudiano.
Hata hivyo Zola alikiri mechi hiyo ya keshokutwa haitakuwa rahisi.
"Itakuwa mechi nzuri na ngumu, sisi tumekuja kutafuta matokeo mazuri, tunajua Raja Casablaca walishinda mabao 3-0, lakini siyo kama wao walishinda basi na sisi itakuwa rahisi hivyo, hizi ni mechi mbili tofauti, naifahamu Simba ni timu nzuri na kubwa Afrika, nawafahamu wachezaji Wakongo wenzangu, Henock Inonga, na yule Jean Baleke ni mdogo wangu nilikuwa naye TP Mazembe," alisema Zola.










