Simba Queens yauota ubingwa

25May 2023
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba Queens yauota ubingwa

BAADA ya kuvuliwa ubingwa, benchi la ufundi la Simba Queens, limesema linajipanga upya kuhakikisha msimu ujao linarudisha kombe lao Ligi Kuu ya Wanawake mikononi mwao.

 

Simba Queens ambayo ilifanya vyema pia katika mashindano ya kimataifa msimu uliopita, imevuliwa ubingwa na JKT Queens kwa tofauti ya pointi moja.

Akizungumza na gazeti la Nipashe jana, Kocha Mkuu wa Simba Queens, Charles Lukula, alisema amesikitika kuona timu yake imepoteza ubingwa msimu huu lakini amekiri ligi ilikuwa na ushindani mkubwa. 

Lukula alisema licha ya kukosa ubingwa anawapongeza wachezaji wake kwa kufanya vizuri na kuongoza kufunga idadi kubwa ya magoli.

"Ingawa hatujapata ubingwa msimu huu lakini timu yangu haijafanya vibaya, sisi ndio tumefunga idadi kubwa ya magoli kuliko timu nyingine, tunaanza kujipanga kwa ajili ya msimu ujao," alisema Lukula.

Kocha huyo alisema atayafanyika kazi mapema mapungufu madogo madogo yaliyojitokeza katika michezo waliyoicheza ili kurejea msimu mpya wakiwa na nguvu zaidi.

"Kuna makosa madogo madogo yaliofanyika katika safu ya ushambuliaji, nitayafanyia kazi mara tu ratiba itakapotoka ili kuanza maandalizi ya msimu ujao mapema," alisema kocha huyo.