Simba Queens kuokoa jahazi la mataji Msimbazi

09May 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba Queens kuokoa jahazi la mataji Msimbazi

MABINGWA Watetezi wa Ligi Kuu ya Soka Wanawake, Simba Queens, leo watashuka Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kucheza dhidi ya Baobab Queens, ikiwa ni mechi muhimu ya kujaribu kuutetea ubingwa wake ambao uko rehani dhidi ya JKT Queens.

Timu hiyo inaweza kuwa ndiyo mkombozi wa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo ambao wametangaza rasmi kumaliza msimu wa 2022/23 bila taji lolote kwa upande wa wanaume.

Hata hivyo, bado Simba Queens inategemea zaidi kupoteza kwa JKT Queens au sare kwenye mechi mbili zilizobaki dhidi ya Fountain Gate Princess na Mkwawa Queens.

Mashabiki wa Simba Queens wanaitegemea zaidi Fountain Gate kuizuia JKT Queens katika mechi kali itakayochezwa kesho kwenye uwanja huo huo wa Jamhuri, lakini hayo yote yatategemea kama itashinda mechi yake ya leo ikiwa ugenini.

Kocha Mkuu wa Simba Queens, Charles Lukula, amesema maandalizi yamekamilika, lakini akikiri ubingwa wa safari hii wa ligi ya wanawake utaamuliwa kwenye mechi ya mwisho.

"Nilisema tangu mwanzo kuwa msimu huu bingwa atapatikana kwenye mechi ya mwisho, timu zote zimekamilika, na zilijiandaa vizuri hasa hizi timu tatu za Simba Queens, Fountain Gate Princess na JKT Queens ziko sawasawa na hata pointi zao hazijapishana sana na ni lazima mechi ya mwisho ndiyo itaamua bingwa.

"Niwaambie tu watu kuwa yeyote atakayekuwa bingwa msimu huu, akienda kucheza michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) pia anaweza kuwa bingwa huko, kwa sababu ametoka kwenye ligi ngumu sana," alisema kocha huyo raia wa Uganda.

Baada ya mechi ya leo, Simba Queens itabakisha mechi moja tu dhidi ya Ceasiaa Mei 17, mwaka huu.

Mpaka sasa JKT Queens ina pointi 40 ikiongoza ligi, Simba Queens 39 nafasi ya pili na Fountain Gate 38 ikiwa nafasi ya tatu.