milango tayari ipo wazi kumnasa beki wa kushoto wa Ihefu FC, Yahya Mbegu.
Simba ni klabu pekee kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki, itakayoshiriki michuano hiyo mikubwa Afrika ambayo inatarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu.
Na kuelekea msimu mpya, Simba imekuwa ikihusishwa na usajili wa Mbegu, ambaye amekuwa katika kiwango bora zaidi msimu huu akiwa na kikosi cha Ihefu FC, na sasa mkataba wake unafikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu na bado hajaanza mazungumzo ya kuongeza kandarasi nyingine na timu yake hiyo.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili ni kwamba nyota huyo tayari ameingia katika rada za Simba na yupo katika rada za viongozi wa Simba kwa ajili ya kuinasa huduma yake kwa msimu ujao.
Akizungumza na Nipashe jana, Mtendaji Mkuu wa Ihefu FC, Zagalu Chalamila, alisema hawana taarifa au ofa kutoka Klabu ya Simba kuhitaji huduma ya Mbegu ambaye mkataba wake unafikia ukingoni baada ya ligi kumalizika.
Alisema nyota huyo yuko katika mipango ya benchi lao la ufundi akiwa miongoni mwa wachezaji ambao wamependekezwa na kocha kusalia ndani ya kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao.
“Mbegu mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, bado hatujaanza kufanya mazungumzo na beki huyo, hatuna haraka naye, kama itatokea timu inamhitaji yeye ndiye ataangalia,” alisema Chalamila.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Simba, Kajula akizungumza na Nipashe jana, alisema wamejipanga kufanya usajili mkubwa baada ya kushindwa kufanya vizuri msimu huu kwa lengo la kuboresha kikosi hicho kinachotarajia kushiriki michuano ya Super League.
"Akili na nguvu zetu ni kuboresha kikosi kwa ajili ya Super League, Simba ni miongoni timu nane katika Bara la Afrika itakayoshiriki michuano hiyo, lazima tufanye usajili mzuri kwa kuboresha kikosi chetu, sasa tunafanya kazi kwa vitendo na si maneno.
"Tumeona msimu huu hatukufanya vizuri, tumeona tatizo la kufanyiwa kazi haraka, tunakutana na mkuu wa benchi la ufundi kwa qjili ya tathmini ya kikosi na mwenendo wa msimu huu na kujadili msimu ujao," alisema Kajula.










