Simba Day haijawahi kutokea

08Aug 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba Day haijawahi kutokea
  • ***Rais Samia aituma mataji CAF, akiahidi tena mamilioni, Onana, Ngoma waiongoza kuirarua Power Dynamos...

KLABU ya Simba jana ilihitimisha kilele cha 15 cha Tamasha la Simba Day katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

 

Hii inakuwa ni mara ya pili kwa Simba kuifunga timu hiyo kwenye kilele cha Simba Day, kwani mwaka 2019 iliichapa mabao 3-1 kwenye uwanja huo.

Kwa ushindi huo, rekodi inayonesha kuwa katika michezo 15 ya tamasha hilo, imeshinda mara tisa, sare mara mbili na kufungwa mara nne.

Walikuwa ni wachezaji wapya kabisa waliosajiliwa msimu huu, Willy Essomba Onana na Fabrice Ngoma waliopeleka furaha Msimbazi kwenye tamasha hilo.

Mapema tu dakika ya nne Onana, raia wa Cameroon aliyesajiliwa kutoka Rayon Sport ya Rwanda alipachika bao baada ya kupokea pasi ndefu  kutoka kwa Mzamiru Yassin akakimbia nao kwenye wingi ya kushoto, akaingia ndani kidogo kabla ya kuachia shuti la mguu wa kulia ukajaa wavuni.

Dakika ya 74, Ngoma aliyesajiliwa kutoka Al Hilal ya Sudan, aliipatia Simba bao la pili dakika ya 74, akiunganisha kwa kichwa krosi ya pembeni kutoka kwa Saido Ntibanzonkiza, ambaye alipigiwa kona fupi na Luis Miquissone.

Katika tamasha hilo ambalo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akihutubia mashabiki 60,000, waliofurika uwanjani hapo jana, ameaziahidi tena klabu zitakazoshiri michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Yanga na Kombe la Shirikisho, Azam FC na Singida Fountain Gate kuwa ahadi yake ya kutoa kiasi cha Sh. milioni tano kwa kila bao moja kama alivyofanya msimu uliopita ipo pale pale.

"Ahadi ipo pale pale, nendeni mkalete ushindi muiletee sifa Tanzania, ahadi ipo pale pale," alisema Rais Samia.

Alizipongeza Simba na Yanga kwa kufanya vema msimu uliopita kwa michuano ya kimataifa huku kuenda kufanya vizuri tena pamoja na Azam FC na Singida Fountain Gate.

 

UTAMBULISHO WA WACHEZAJI

Ulianza saa 10: 36 huku kubwa ikiwa ni zawadi ambayo haikutarajiwa na mashabiki utambulisho wa kipa mpya mzawa kutoka KMC FC, Hussein Abel, ambaye anaungana na makipa wengine wa klabu hiyo akiwamo Ahmed Feruz, Ally Salim na Aishi Manula.

Mabeki Shomari Kapombe, David Kameta, Jimmyson Mwanuke, Mohamed Hussein, Israel Patrick, Kennedy Juma, Hussein Kazi, Che Fondoh Malone na Henock Inonga Bacca.

Viungo ni Abdallah Hamis, Mzamiru Yasin, Sadio Kanoute, Nassoro Kapama, Fabrice Ngoma, Clatous Chama, Willy Essomba Onana, Aubin Kramo, Peter Banda, Saido Ntibazonkiza, na Kibu Denis huku washambuliaji wakiwa ni Shaban Chilunda, John Bocco, Mohamed Musa, Jean Baleke, Moses Phiri na Luis Miquissone.

Jumla ya wachezaji 30 wametambulishwa ambao wataitumikia Simba kwa msimu mpya wa 2023/24 na benchi la ufundi likiendelea kuwa chini ya Robertinho Oliveira.

Hili ni tamasha la 15 kufanywa na Simba tangu lilipoasisiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wao, Mzee Hassan Dalali, pamoja na Katibu Mkuu mkuu wake, Mwina Kaduguda. Nahodha Msaidizi, Mohamed Hussein 'Tshabalala', ndiye mchezaji mwandamizi zaidi kwenye kikosi cha Simba hivi sasa akiwa amedumu kwa misimu tisa tangu aliposajiliwa mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar, hiyo ikiwa ni Simba Day yake ya 10.

 

 

REKODI KUINGIA UWANJANI:

Tamasha la Simba Day mwaka huu limeweka rekodi ya kujaza uwanja zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya mchezo, na juzi mageti ya uwanjani hapo yalifunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi ili kupunguza msongamano wa watu kuingia na kufika saa 4:30 asubuhi tayari upande wa viti vya mzunguko vilikuwa vimeanza kujaa.

Hadi saa 6:00 mchana jukwaa la  viti vya Orange mashabiki waliingia na kujaza nafasi hiyo, kufika saa 7:30 mchana uwanja ulikuwa umejaa.

 

MCHEZO WA KIRAFIKI TIMU YA WANAWAKE NA VIJANA:

Timu ya Simba Queens ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Masala Princess ambapo Malkia wa Wekundu wa Msimbazi hao waliibuka na ushindi wa mabao 4-0, yakifungwa na Asha Djafari aliyetupia mawili huku Joelle Bukuru na Shelda Boniface kila mmoja akifunga moja.

Kwa upande wa mechi ya vijana walicheza wenyewe kwa wenyewe huku timu ya kwanza ikipewa jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan na nyingine ikipewa jina la Makamu wa Rais Dk. Phillip  Mpango.

Timu ya Rais Samia ikiwa imevalia jezi za  rangi nyeupe ikinolewa na Selemani Matola na ya Makamu Rais, Dk. Mpango ilivaa uzi wa rangi nyekundu. Kikosi kilichopewa Samia Boys kiliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mpango Boys.

 

BURUDANI KUANZA:

Saa 5:35 asubuhi Burudani ya Muziki ilianza baada ya wasanii mbalimbali kupanda katika jukwaa maalum kwa ajili ya kuburudisha mashabiki 60,000 waliopo uwanjani.

Saa 6:17 mchana Bendi ya Twanga Pepeta inayomilikiwa na Mjumbe wa Bodi ya Simba, Asha Baraka ilitoa burudani kwa kuimba nyimbo ya ‘Angurumapo Simba’ ambayo ilikuwa kivutio cha mashabiki uwanjani hapo.

Wasanii mbalimbali walitoa burudani akiwamo John Simon ‘Joh Makini’ na Meja Kunta, huku Tunda Man akitia fora kwenye tamasha hilo kwa kuingia kwa staili ya mfungwa na kibao chao cha 'Simba Sihami'.

Kikundi cha Sarakasi cha jijini Mwanza kilipanda Jukwaani saa 9:18 na kutoa burudani.

Ally Saleh ‘Ali Kiba’, ni msanii wa mwisho katika orodha ya watu waliotoa burudani ambapo alipanda jukwaa saa 9:37 na kukata kiu ya mashabiki waliojitokeza kwa wingi kushuhudia kikosi kipya cha 'Wekundu wa Msimbazi' hao wa msimu huu unaotarajiwa kuanza Agosti 9, mwaka huu.

 

MENEJA WA IDARA YA HABARI NA MAWASILIANO AFUNIKA

Saa 10 :00 alasiri Ahmed Ally alifunika baada ya kuingia uwanjani na Ngamia kwa ajili ya kutambulisha wachezaji na benchi la ufundi.

 

Wachezaji Simba wanena:

Kiungo wa timu hiyo, Clatous Chama, alisema msimu huu wamejipanga kivingine kwa kila mchezaji kuhitaji kurejesha heshima ya klabu hiyo kwa kutwaa mataji ya ndani.

Alisema kwa muda ambao wako kambini kwa wale waliokuwapo msimu uliopita na wachezaji wapya wamekuwa na muunganiko mzuri na anaimani kufikia malengo yao kwa msimu wa 2023/24.

“Tunatakiwa kupambana kurudisha ubingwa wetu msimu huu, pia tuna kazi kubwa iliyopo mbele yetu kuvuka katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kucheza nusu au fainali.

Beki wa timu hiyo, Che Fondoh Malone, alisema rangi pendwa kwake ni nyekundu na nyeupe ambayo anaamini Simba kwake ni sehemu sahihi na anaimani atafanya kile ambacho viongozi walishawishi kumsajili.

“Sitawaangusha benchi na viongozi kwa kunisajili, kikubwa tunahitaji kuwapa furaha mashabiki wetu wa Simba, kutwaa mataji na kufanya vizuri, ninaimani nimekuja kuimarisha 'Ukuta wa Yeriko' ndani ya timu yangu mpya,” alisema Che Malone.