Taarifa hiyo imekuja siku chache baada ya mechi kati ya Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Uganda kusimama kwa zaidi ya dakika 30 kutokana na jenereta lililokuwapo kushindwa kuwasha taa na kuleta sintofahamu.
Akizungumza jijini jana, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Pindi Chana, alisema kwa sasa wameshaanza mchakato wa kuboresha uwanja huo ili kuwa wa kisasa kama vilivyo viwanja vya nchi zilizoendelea.
Chana alisema pia serikali iko katika mchakato wa kuboresha viwanja vilivyoko katika mikoa ya Mbeya, Tanga, Dodoma na Arusha ili kuhakikisha wanakuwa na viwanja bora zaidi vya michezo.
"Tuko na mikakati ya kuboresha uwanja wetu wa Benjamin Mkapa kuwa bora zaidi ya sasa, baadhi ya viwanja mikoani na kujenga viwanja vya mazoezi katika eneo la Kawe,” alisema Chana.
Waziri huyo alisema pia serikali inaangalia changamoto mbalimbali zinazowakuta wanamichezo ikiwamo suala la mikataba ya wachezaji na ufanisi wa viongozi kuhakikisha michezo inazidi kufanya vizuri.
"Suala la mikataba ya wachezaji litasimamiwa kwa umakini na kuweka mikakati ya nyota hao kupata haki zao za msingi, kulipwa vizuri lakini pia timu zinatakiwa kufanya vizuri katika michuano iliyopo mbele yao kama ilivyo kwa Simba na Yanga," Chana alisema.
Aliongeza wanajipanga kuona sekta ya michezo Tanzania inakua kwa kasi lakini pia kuboresha kwenye utamaduni kwa kuzungumza na taasisi na benki mbalimbali kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wasanii.
Naye Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao, alisema changamoto kubwa inayofanya michezo kutosonga mbele hapa nchini ni kukosekana kwa miundombinu bora ikiwamo viwanja vya kisasa.
Kidao alisema Tanzania haina viwanja vya kutosha ambavyo ni bora kwa ajili ya kumfundisha mtoto kuanzia umri wa chini na timu za ligi kutokuwa na viwanja wa mazoezi ambavyo vinamilikiwa na klabu hizo ni tatizo lingine.
“Lazima mtoto anatakiwa kujifunza katika kiwanja bora kwa kuanza kufundishwa mpira, lakini pia kuwapo kwa sera nzuri katika michezo shuleni kama ilivyokuwa zamani tulipokuwa tukisoma na kupata nafasi ya kufanya michezo shuleni,” alisema Kidao.










