Lengo ya ushirikiano huo ni kuhakikisha ligi hiyo inatangazwa vyema na kuwavutia wafanyabishara na makampuni mbalimbali kuwekeza.
Hayo yalisemwa katika mkutano wa majadiliano kati ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na wadau wa sekta binafsi yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Pindi Chana, alisema anaamini ushirikiano huo utaiwezesha ligi hiyo kupata wadhamini wengi na hatimaye kuchezwa kwa ufanisi zaidi.
Chana pia, alisema ametoa agizo kwa Naibu wake, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, kufikisha ombi la ongezeko la bajeti katika sekta ya michezo kwa mwaka mpya wa fedha.
Alisema, wizara hiyo imejipanga kuhakikisha maendeleo katika kila sekta iliyopo chini yao inafanya vyema ikiwamo kuwapa nafasi makocha kupata elimu ya juu nje ya nchi ili kuja kufundisha Timu za Taifa pamoja na kutengeneza fursa za kwenda kufundisha nje.
“Tunahitaji kuona Utamaduni na Sanaa nao hawako nyuma kufanya maendeleo katika taifa letu, kufikia huko lazima tuwe na fungu la kutosha, nimemwagiza naibu wangu kupeleka bungeni maombi ya kuongezewa bajeti yetu kwa mwaka huu wa fedha. Tunahakikisha wizara hatui vikwazo vya kukwamisha sekta hii," alisema waziri huyo.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, alisema inasikitisha Ligi Kuu ya Wanawake inakosa wadhamini wakati katika sekta ya michezo, soka la wanawake ndio linafanya vizuri kimataifa.
Msitha alisema BMT wanaliangalia soka la wanawake kwa jicho la tatu na wanaendelea kushirikiana na TFF ili kuitangaza ligi hiyo kwa kuyashawishi makampuni makubwa kudhamini ligi hiyo.
Aliongeza Ligi Kuu ya Wanawake imekuwa kivutio kikubwa na kwa sasa zinapokutana timu pinzani ( Simba Queens na Yanga Princess), wanaonyesha kandanda safi zaidi ya mpira wa wanaume.










