Msemaji wa Yanga, Jerry Muro alisema jana kuwa timu yao inaondoka leo asubuhi kwenda Tanga na safari ya Afrika Kusini iliyokuwa ifanyike kesho haitakuwapo tena.
Muro alisema baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuitolea nje timu hiyo kwenda Bondeni kuweka kambi ya siku nane kujiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa wamehamishia nguvu kwenye mchezo wa Jumamosi.
"Timu inakwenda Tanga kesho (leo), safari ya Afrika Kusini haipo tena," alisema kwa kifupi Muro.
Mapema jana asubuhi, kiongozi mwingine wa juu wa Yanga aliliambia gazeti hili kuwa safari hiyo isingewezekana.
"Maombi yetu yalionekana kama tumekurupuka, kwa ufupi safari hii haipo tena," alisema kiongozi huyo bila kutaka jina lake kuandikwa kwenye gazeti.
Hata hivyo alisema kama safari hiyo ingefanikiwa, wangepata faida kubwa ya maandalizi kwa ajili ya michuano ya kimataifa.
"Safari ya Afrika Kusini haipo, timu inaelekea Tanga kesho (leo) na wachezaji wetu tumeshawataarifu."
Mchezaji mwingine mkongwe wa timu hiyo (jina tunalihifadhi) alisema safari ya Afrika Kusini wanaisikia kwenye vyombo vya habari, lakini anachofahamu kuna safari ya Tanga.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu waliibuka na safari yao ya Sauzi ikiwa ni siku moja baada ya Azam FC kupata ruhusa ya kwenda Zambia kushiriki mashindano maalum yaliyoandaliwa kwa kushirikisha timu nne.
Kufuatia ziara hiyo ya Azam, TFF lilitangaza kuahirisha mechi mbili za ligi zinazoihusu timu hiyo ambayo mwezi ujao itaanza hekaheka ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo, jana mchana Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa TFF, Baraka Kizuguto alisema hakuna barua iliyotumwa na Yanga kuomba ruhusa ya kwenda Sauzi na kwamba kilichokuwa kikizungumzwa na Yanga ni habari za mtaani.










