Simba imerejea nchini jana kutokea Morocco kwenye mchezo wao wa kukamilisha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablaca ambao ilikubali kipigo cha mabao 3-1, lakini hata hivyo, timu hizo zote zilishafuzu robo fainali katika Kundi lao la C.
Akizungumza na Nipashe baada ya kutua nchini, Robertinho, alisema mechi hizo mbili ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea mchezo wao wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ambapo mpinzani wao watamjua keshokutwa, Jumatano.
Robertinho alisema mechi mitatu za nyumbani ikiwamo michezo miwili dhidi ya Ihefu FC mchezo wa Kombe la FA na mechi ya Ligi dhidi ya Yanga ataitumia kwa ajili ya kujiandaa na michezo yao miwili ya robo fainali.
Alisema wachezaji wake hawakucheza vibaya kwenye mechi iliyopita dhidi ya Raja Casablanca na kwamba walicheza vizuri na kuonesha kiwango kizuri, licha ya kufungwa.
“Nimefurahi kuona Simba imefuzu kucheza hatua ya robo fainali licha ya kupoteza mchezo dhidi ya Raja Casablanca, sasa akili na nguvu tunazielekeza kwenye mechi zilizopo mbele yetu ikiwa ni pamoja na kushinda dhidi ya Yanga na kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.
"Kuhusu wachezaji wangu wawili Mohammed Hussein (Tshabalala) na Sadio Kanoute ambao hawakuwapo mechi iliyopita, sasa nitaungana nao kuelekea mechi zetu zijazo kuhakikisha tunafikia malengo,” alisema Robertinho.
Katika hatua nyingi Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, akikabidhi zawadi ya Sh. milioni tano ikiwa ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutoa kiasi hicho kwa kila goli litakalofungwa na Simba na Yanga kwenye michuano ya kimataifa msimu huu, alisema amekabidhi fedha fedha hizo ikiwa utekelezaji ya Mama.
“Nimekuja kukabidhi hizi fedha nina imani itakuwa chachu kwa wachezaji kuendelea kufanya vizuri katika hatua inayofuata ya robo fainali,” alisema Msigwa.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alimshukuru Rais Samia na kumuahidi kupambana kuhakikisha wanampeleka Mama nusu fainali.
Aliongeza kuwa baada ya droo ya Jumatano watamfahamu mpinzani wao na Aprili 21 au 22, mwaka huu, wataanza kutupa karata yao katika hatua ya robo fainali.
“Tunamkaribisha Mama Aprili 21 au 22, kuja kuwashuhudia watoto wake wakipambana, lakini kuja kuwakabidhi fedha kwa mikono yake katika mchezo wetu wa kwanza wa robo fainali tutakaocheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam,” alisema na kuongeza:
"Safari yetu ilikuwa sehemu kubwa na mambo mengi, lakini tunamshukuru Mungu tumefika na tumecheza mechi bora sana hasa jinsi ya wachezaji walicheza vizuri.
"Licha ya kupoteza mechi tumeridhika, hivyo tumejifunza na tunajua jinsi gani ya kucheza, sasa tunasubiri droo ipangwe, maana tunayemtamani na sisi anatutamani,” alisema Ahmed.
Aidha, Ahmed alisema hali ya Shomari Kapombe imeimarika, lakini anatakiwa kufanyiwa vipimo zaidi ili kujua ameumia kwa kiasi gani na siku atakayorejea uwanjani.
Alisema wchezaji wamepewa mapumziko ya siku chache na ndani ya siku mbili hizi, wataingia kambini kujiandaa na mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Ihefu FC itakayopigwa Ijumaa wiki hii katika Uwanja wa Uhuru na baadaye kurudiana nao Mbarali, Mbeya kwenye mchezo wa Ligi Kuu kabla ya Aprili 16, mwaka huu kuvaana na Yanga.










