Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kocha huyo amesema watakwenda na mfumo wao ambao anaamini utampa matokeo mazuri lakini watakuwa na nidhamu kubwa kwenye mchezo huo na watakachowapa Power Dynamos ni 'Suprise'.
"Katika mechi yetu ya ugenini tutakwenda kucheza tofauti na tutakavyocheza nyumbani, huko tutakuwa na nidhamu kubwa ya ukabaji, kutakuwa na msitari mmoja wa mabeki, mwingine ni wa viungo wakabaji na viungo washambuliaji wote itabidi wacheze pamoja, tutacheza kwa kukaribiana na kuufinya uwanja na kama kwenye kushambulia tutakwenda kwa pamoja na kurejea haraka, baada ya hapo katika mechi ya marudiano tutaangalia nini tutafanya, lakini nyumbani tutataka kucheza kwa uhuru kila mchezaji akionyesha kipaji chake kwa sababu soka si vita ila ni sanaa," alisema Robertinho.
Aidha, kocha huyo alisema anaandaa mkakati wa kuhakikisha wachezaji wake wanatumia nafasi zinazopatikana kwani amegundua wanatengeneza nyingi lakini wanashindwa kuzitumia.
"Tumecheza mechi mbili za ligi, ila mechi tulioshinda mabao 2-0 tulikosa mabao mengi tukiwa ndani ya boksi, Simba ni timu kubwa inatakiwa kucheza vizuri na kushinda mechi ikitumia nafasi zinazopatikana, hilo tunalifanyia kazi," alisema Robertinho.
Aidha, Robertinho alisema kikosi chake kinatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki na kama mambo yakienda vizuri huenda kesho Jumamosi ikateremka dimbani.
"Tunataka kulinda utimamu wa mwili na pumzi za wachezaji wetu baada ya 'pre season' ya nchini Uturuki, kwa maana hiyo nadhani tutakuwa na mechi kama mbili za kirafiki, Jumamosi ijayo, Jumatatu au Jumatano, na nafikiri tutapata timu nzuri za kutupima kwa sababu tuna michuano mingi, Ligi ya Mabingwa tukiingia hatua ya makundi na African Super League tutakuwa na mechi nyingi, kwa hiyo ni lazima tujiandae vizuri," alisema.
Katika hatua nyingine uongozi wa Simba upo kwenye mchakato wa kutafuta nchini jirani au sehemu sahihi ndani ya nchi kwa ajili ya kwenda kuweka kambi ya muda mfupi kabla ya kucheza mechi ya kwanza ya msimu wa 2023/24 ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.
Hatua hiyo ni kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa ili na kufikia malengo yao msimu huu ya angalau kucheza hatua ya nudu fainali.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema Kenya ni moja ya nchi ambayo imekuwa ikitajwa na menejimenti ili kwenda nchini humo kuweka kambi ya muda mfupi.
Simba itacheza na Power Dynamos Agosti 16 kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania nafasi ya kuingia hatua ya makundi.
*Imeandaliwa na Saada Akida na Adam Fungamwango









