Mechi hiyo ya fainali inayosubiriwa kwa hamu imepangwa kupigwa Mei 28 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mechi ya mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema tiketi hizo ni mwendelezo wa kuongeza hamasa, ikiwa ni baada pia ya kuahidi Sh. milioni 20 katika kila bao la ushindi litakalofungwa na wachezaji wa Yanga kwenye mechi hizo mbili za fainali.
“Rais Samia anahakikisha kuwa Yanga inachukua kombe kwa kuendeleza hamasa hizi za kununua tiketi 5,000 kwa lengo la kuujaza Uwanja wa Taifa utakaoshuhudia mchezo mgumu wa fainali kati ya timu ya Tanzania ya Yanga dhidi ya USM Alger.
“Rais anawataka Watanzania waende kuujaza uwanja kwa sababu mama hana mbambamba katika mbio za Yanga kuitangaza nchi kimataifa kupitia mpira wa miguu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Msigwa aliwataka wachezaji kuingia uwanjani kwa nguvu zote ili washinde magoli mengi kwa sababu fedha za Rais zinazotolewa ili kuibua hamasa bado zipo kwa lengo moja la kuhakikisha Yanga inaibuka kidedea katika mechi zake za fainali za Kombe la Shirikisho.
Mechi ya marudiano kati ya Yanga na USM Alger inatarajiwa kupigwa nchini Algeria, Juni 3, mwaka huu, huku Yanga ikiingia fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano ya Kimataifa inayoendeshwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika.
Mengine makubwa yaliyofanywa na Rais Samia dhidi ya Yanga katika mechi yao ya fainali ni kuipa ndege klabu hiyo ili iende Algeria katika mechi yao ya marudiano.
Yanga imekuwa kwenye kiwango bora msimu huu ikifanikiwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu na kuingia kwenye fainali mbili za kombe la Shirikisho la TFF na lile la CAF.










