Imetajwa na makocha wa timu hizo kuwa soka lao la nguvu ni changamoto kwa timu zao lakini pia wamedai kuwa hayo ni matunda ya maandalizi mazuri ya Ligi Kuu msimu huu.
Prisons ikiwa nyumbani Mbeya ilivuna pointi tano kutoka kwa Simba, Yanga na Azam. Waliifunga Simba mzunguko wa kwanza msimu huu kwa magoli 1-0, magoli lililofungwa na Mohamed Mkopi.
Yanga nayo ililazimisha sare ya magoli 2-2, mabao ya Mkopi na Jeremiah Juma wakati Yanga ilipata magoli Simon Msuva pamoja na Amissi Tambwe. Kwenye mechi ya Prisons dhidi ya Azam iliisha kwa sare ya 0-0.
Kocha wa Simba, Jackson Mayanja alisema, “Kuna timu 15 ambazo kwa msimu huu zilikuwa zicheze dhidi ya Simba lakini ninayoiona kuwa ni timu ngumu zaidi ni Prisons kutokana na uimara wa wachezaji wao.
“Pia uwezo wao unatokana na mbinu ambazo anazitumia kocha wao anapokuwa akikutana na timu mbalimbali,” alisema kocha huyo raia wa Uganda.
Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans Van Der Pluijm, “ Kila timu huwa inajiandaa kwa staili yake na kujipanga kucheza wanavyojua. Kiukweli Prisons ni moja ya timu inayotoa changamoto kubwa kwa msimu huu. Wamejiandaa vizuri na hiko ndicho kinachowabeba.
“Huwa wanacheza mpira wa nguvu na ni staili ambayo inakubalika kwenye soka sema tu wanavyocheza wanatakiwa kuzingatia sheria na kucheza kiungwana.
Kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall alisema kuwa hajacheza na timu inayocheza mpira wa nguvu kama hiyo. “Kucheza na Prisons ni kama vita. Ni ngumu kupata matokeo mbele yake kwani wanacheza kwa nguvu sana.”
Hata hivyo, Kocha wa Prisons, Salum Mayanga alisema, “Wanaosema kuwa ninawachezea soka la nguvu wanapaswa kutambua kuwa soka si kazi rahisi.
“Ili timu zifanikiwe kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa zinapaswa kujiandaa kwa kila mbinu ikiwemo kukabiliana na timu zinazocheza soka la nguvu,” alisema.










