Prisons iko nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza michezo 14, imeshinda minne imetoka sare tano na kupoteza mitano.
Kocha wa Prisons, Hamad Ally, alisema wameamua kuweka kambi Kiwira kwa sababu ya kupata utulivu wa kujiandaa vizuri na ligi.
“Kwanza tumeona kuna mazingira magumu ya kutumia uwanja wetu wa nyumbani (Sokoine Mbeya) kwa sasa kwa sababu una matumizi mengi, timu nyingi zinatumia zikiwamo za vijana, daraja la kwanza na mambo ya kijamii hivyo kuna mwingiliano sana tukaona tutakosa utulivu.
“Ndio maana tukaamua kuja kujichimbia Tukuyu ingawa mwanzo tulitamani kuweka kambi ya nje ya mkoa wetu, lakini kutokana na mazingira imekuwa changamoto kwetu.
“Tumeona kwa sasa huku Mbeya kuna baridi tukisema tutoke na kuweka kambi mikoa mingine ambayo kwa sasa ina joto ingetupa shida,“ alisema Ally.
Akizungumzia usajili wa timu hiyo kwenye dirisha dogo, Ally alisema ameamua kuongeza wachezaji wengi wa nafasi ya ushambuliaji kwa sababu anataka mabao.
Prisons imeongeza wachezaji sita kwenye dirisha dogo, lakini washambuliaji wakiwa wengi zaidi. Imewasajili washambuliaji Tariq Simba, George Sangija (Geita Gold) Abdulkarim Segeja (Copco), Jacob Benedictor (Mbeya Kwanza), Ally Msengi (Moroka Swallows) na beki Feisal Mfuko kutoka Majimaji.
“Tumeona eneo la ushambuliaji ndio linahitajika kuongeza nguvu kubwa zaidi kwa sababu tunataka mabao mengi yatakayotupatia pointi kwenye ligi,“ alisema.