Pluijm atoboa siri Yanga kuboronga

05Feb 2016
WAANDISHI WETU
Nipashe
Pluijm atoboa siri Yanga kuboronga
  • **Timu hiyo ya Jangwani imeambulia pointi moja tu katika mechi zote mbili zilizopita za duru la pili la ligi ya Bara.

WAKATI huzuni ikianza kuiandama mitaa ya Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam kutokana na Yanga kuuweka rehani ubingwa wa ligi ya Bara msimu huu, kocha wa timu hiyo, Hans van der Pluijm, ameweka wazi changamoto zinazoikabili timu yake.

Timu hiyo ambayo iliuanza vibaya mzunguko wa pili wa ligi hiyo msimu huu kwa kufungwa 2-0 na kuandikisha kipigo cha kwanza dhidi ya Coastal Union tangu 2007, imeendelea kusuasua katika mbio za ubingwa baada ya juzi kuambulia pointi moja ilipotoka sare ya 2-2 dhidi ya Tanzania Prisons mjini Mbeya.
Sare hiyo iliwafanya wawe na pointi moja mbele ya mahasimu wao wa jadi, Simba ambao wamepanga kuutumia msimu huu kumaliza ukame wa mataji Msimbazi.
Wakati kila mtu anaongea lake kuhusu kuboronga kwa Yanga katika mechi mbili zilizopita, Pluijm jana aliweka wazi changamoto zinazoikabili timu yake ambayo mwaka huu inaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
"Tatizo letu kwa sasa na kuwa na wachezaji wengi ambao ni majeruhi," Pluijm alisema. "Najua mashabiki wetu wanajisikia vibaya kwa matokeo haya, hata benchi la ufundi hatufurahishwi na mwenendo huu.
"Pia kuna changamoto ya viwanja, tunacheza mpira wetu wa pasi za uhakika tunapocheza kwenye Uwanja wa Taifa, imekuwa ngumu kwetu kucheza vizuri kwenye viwanja vya nje ya Dar es Salaam kwa sababu (viwanja) vingi ni vibovu."
Beki wa pembeni kushoto Hajji Mwinyi Mngwali anauguza majeraha pamoja na nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' ambaye hajacheza mechi hata moja tangu Desemba alipoumia goti huku beki wa kati asiyekosa penalti Kelvin Yondani akitakiwa kukosa mechi mbili baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Coastal.
Huku akichanganya na 'umombo' kidogo wakati akizungumzia mechi hiyo, kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Salum Mayanga, alionekana kuponda kiana uchezeshaji wa refa wa kati Florentino Zablon kutoka Dodoma aliyesaidiwa na Charles Simon (Dodoma) na Mohamed Mkono (Tanga).
"Siwezi kuzungumzia uchezeshaji wa marefa, lakini mwamuzi wa 'Champions League' (Ligi ya Mabingwa) anatakiwa kupewa mtihani wa 'Champions League'," Mayanga aliwaambia waandishi wa habari mara tu baada ya kumalizika kwa mechi hiyo.
Mwajiriwa huyo wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amekuwa kocha wa kwanza kupata pointi nne kutoka kwa klabu kongwe nchini, Simba Yanga baada ya kuwafunga bao 1-0 Wanamsimbazi mjini Mbeya Oktoba 21 katika mechi yao ya duru la kwanza.
Hadi sasa Yanga yenye pointi 40 kileleni mwa msimamo, imecheza mechi saba nje ya Dar es Salaam ikipoteza moja dhidi ya Coastal, imeshinda tatu dhidi ya Mtibwa (Morogoro), Kagera (Tabora) na African Sports (Tanga), sare tatu dhidi ya Mwadui (Shinyanga), Mgambo (Tanga) na Prisons.

Imeandikwa na Nebart Msokwa na Sanula Athanas (Dar)